Tumsifu Yesu Kristo. Karibu Katika Masomo ya Misa 13/08/2024
2024 AGOSTI 13: JUMANNE-JUMA LA 19 LA MWAKA
Mt. Ponsian, Papa na Hipoliti, Padre na Mashahidi
Rangi: Kijani
Zaburi: Juma III
Somo 1. Eze 2:8-3:4
Ezekieli aliisikia sauti, ikamwambia: mwanadamu, sikia neno hili ninalokuambia; usiwe wewe mwenye kuasi kama nyumba ile yenye kuasi; funua kinywa chako, ule nikupacho. Nami nilipotazama, mkono ulinyoshwa kunielekea; na tazama, gombo la chuo lilikuwa ndani yake. Akalikunjua mbele yangu; nalo lilikuwa limeandikwa ndani na nje; ndani yake yalikuwa yameandikwa maombolezo, na vilio, na ole! Akaniambia, mwanadamu, kula uonacho; kula gombo hili, kisha enenda ukaseme na wana wa Israeli. Basi nikafunua kinywa changu, naye akanilisha lile gombo. Akaniambia, “Mwanadamu, lisha tumbo lako, ulijaze tumbo lako kwa hili gombo nikupalo. Ndipo nikalila, nalo kinywani mwangu lilikuwa tamu, kama utamu wa asali. Akaniambia, mwanadamu, haya! Waendee wana wa Israeli,” ukawaambie maneno yangu. |
Wimbo wa Katikati. ” Zab 119:14, 24, 72, 103, 111, 131″
1. Nitalitangaza jina Bwana; (K) Mausia yako matamu sana kwangu. 2. Kumbuka siku za kale, 3. Yeye Aliye juu alipowapa mataifa urithi wao, 4. Bwana peke yake alimwongoza, |
Injili. Mt 18:1-5, 10, 12, 14
Wanafunzi walimwendea Yesu wakisema, “Ni nani basi aliye mkuu katika ufalme wa mbinguni?” Akaita mtoto mmoja, akamweka katikati yao, akasema, “Amin, nawaambia, Msipoongoka na kuwa kama vitoto, hamtaingia kamwe katika ufalme wa mbinguni. Basi, ye yote ajinyenyekeshaye mwenyewe kama mtoto huyu, huyo ndiye aliye mkuu katika ufalme wa mbinguni. Na ye yote atakayempokea mtoto mmoja mfano wa huyu kwa jina langu, anipokea mimi. Angalieni msidharau mmojawapo wa wadogo hawa; kwa maana nawaambia ya kwamba malaika zao mbinguni sikuzote huutazama uso wa Baba yangu aliye mbinguni. Mwaonaje? Mtu akiwa na kondoo mia, mmoja akampotea, je, Hawaachi wale tisa na tisini, akaenda milimani, na kumtafuta yule aliyepotea?” Vivyo hivyo haipendezi mbele za Baba yenu aliye mbinguni kwamba mmoja wa wadogo hawa apotee. |
TAFAKARI
TUJIKABIDHI MIKONONI MWA MUNGU: Mungu anatutaka tuyafahamu mausia yake tupate kuwafahamisha wengine. Ezekiel anaambiwa ale, maana yake asome na kutafakari kwa kina mausia ya Mungu, na tukisha fahamu na kuwa na nguvu atutume kuwalisha wengine kwa mafunuo tunayoyafahamu. Utume wa malezi katika Kanisa umekuwa mgumu kwa sababu wengi hatutengi muda kusoma na kutafakari Neno la Mungu kwa kina. Tufahamu kuwa neno hilo, “Ni hai, lina nguvu, na linafahamu mpango wa Mungu kikamilifu” (Ebr 4:12-13). Tutenge muda kwa ajili ya Neno la Mungu. Katika injili ya leo, Kristo anaweka mbele yetu utaratibu wa kufika katika utukufu wa Mungu Baba. Mwaliko ni kuwa wanyenyekevu, kujiachia mikononi mwa Mungu na kutegemea neema na huruma yake. Tuepe majivuno ya namna yeyote yanayotokana na nafasi tulizojaliwa kwa ajili ya huduma za Kanisa au za kijamii. Aidha, kama watoto wadogo, tuwe daima tayari kuongoka na kumrudia Mungu kwa unyofu wa moyo. SALA: Ee Bwana utupe moyo ulio mnyofu kama watoto wadogo. |