Somo 1. Eze 18:1-10, 13, 30-32
Neno la Bwana likanijia tena kusema, je! Maana yake ni nini hata mkatumia mithali hii katika Israeli, mkisema, Baba wamekula zabibu mbichi, nao watoto wakatiwa ganzi la meno? Kama mimi niishivyo, asema Bwana Mungu, hamtakuwa na sababu ya kuitumia tena mithali hii katika Israeli. Tazama, roho zote ni mali yangu; kama vile roho ya baba ni mali yangu, ndivyo ilivyo roho ya mwana mali yangu, roho ile itendayo dhambi itakufa. Bali kama mtu ni mwenye haki, na kuyatenda yaliyo halali na haki; hakula juu ya milima, wala hakuviinulia macho vinyago vya nyumba ya Israeli, wala hakumtia unajisi mke wa jirani yake, wala hakumkaribia mwanamke wakati wa kutengwa kwake; wala hakumdhulumu mtu, bali amemrudishia mdeni wake rehani yake, wala hakumnyang’anya mtu mali yake kwa nguvu, naye amewapa wenye njaa chakula chake, na kuwavika nguo walio uchi; ambaye hakumkopesha mtu ili apate faida, wala hakupokea ziada ya namna yo yote; naye ameuepusha mkono wake na uovu, na kufanya hukumu ya haki kati ya mtu na mwenzake; tena ikiwa amezifuata sheria zangu, na kuzishika hukumu zangu; mtu huyu ni mwenye haki; hakika ataishi, asema Bwana Mungu. Walakini akizaa mwana aliye mnyang’anyi, mmwaga damu, atendaye mambo hayo mojawapo, naye amekopesha watu ili apate faida, na kupokea ziada; je! Ataishi baada ya hayo? La, hataishi; amefanya machukizo hayo yote; hakika atakufa; damu yake itakuwa juu yake. Basi, nitawahukumu ninyi, nyumba ya Israeli, kila mmoja kwa kadiri ya njia zake, asema Bwana Mungu. Rudini, mkaghairi, na kuyaacha makosa yenu yote; basi hivyo uovu wenu hautakuwa uharibifu wenu. Tupilieni mbali nanyi makosa yenu yote mliyoyakosa; jifanyieni moyo mpya na roho mpya; mbona mnataka kufa, enyi nyumba ya Israeli? Maana mimi sikufurahii kufa kwake afaye, asema Bwana Mungu; basi ghairini, mkaishi. |
Wimbo wa Katikati. Zab 51:12-15, 18-19
1. Ee Mungu, uniumbie moyo safi, Uifanye upya roho iliyotulia ndani yangu. Usinitenge na uso wako, Wala roho yako mtakatifu usiniondolee. (K) Ee Mungu, uniumbie moyo safi. 2. Unirudishie furaha ya wokovu wako; Unitegemeze kwa roho ya wepesi. Nitawafundisha wakosaji njia zako, Na wenye dhambi watarejea kwako. (K) 3. Maana hupendezwi na dhabihu, au ningeitoa, Wewe huridhii sadaka ya kuteketezwa. Dhabihu za Mungu ni roho iliyovunjika; Moyo uliovunjika na kupondeka, Ee Mungu, hutaudharau. (K) |
Injili. Mt 19:13-15
Yesu aliletewa watoto wadogo ili aweke mikono yake juu yao na kuwaombea; wanafunzi wake wakawakemea. Lakini Yesu akasema, Waacheni watoto wadogo waje kwangu; wala msiwazuie; kwa maana walio mfano wa hao, ufalme wa mbinguni ni wao. Akaweka mikono yake juu yao, akatoka huko. |
TAFAKARI
TUWAPELEKE WATOTO KWA YESU: Kati ya changamoto tunazokutana nazo ni pamoja na kuyumba kwa uchumi, ukosefu wa ajira, uaminifu kati ya ndugu na marafiki, magonjwa n.k. Kwa kinywa cha nabii Ezekiel, Mungu anataka tuache kulaumiana, kila mmoja ajichunguze, amechangia vipi hali ilivyo. Watu wakitimiza wajibu kikamilifu na kwa unyofu, hakutakuweko na kulaumiana. Watu wameacha unyofu na uadilifu katika utendaji. Je, tunatarajia changamoto ziishe kwa namna gani? Tuwe wanyofu katika utendaji, kila mmoja afahamu kuwa yeye ndiye mtendaji na anayeweza kuleta mabadiliko chanya. Katika Injili wazazi wanawaleta watoto kwa Yesu kwa ajili ya baraka lakini wanafunzi wake. Hakuwa wanaelewa utume wa Yesu. Hata leo, kuna tabia ya kuwazuia watoto kumfikia Yesu mapema. Wengine wamekatazwa kujiunga na mashirika ya kitume na wanacheleweshwa mafundisho ya Komunyo ya kwanza na Kipaimara. Tamko la Yesu ni hili msiwazuie. Waacheni watoto wamfikie na kujifunza misingi ya maisha mapema, ndipo tutapata watu wanyofu wenye dhamiri zilizoundwa.
SALA: Ee Mungu uwajalie wazazi watimize wajibu wao wa kuwapeleka watoto kwako. |