Somo 1. Eze 16:59-63 Au Eze 16:1-15, 60, 63
Bwana Mungu asema hivi; Nitakutenda vile vile kama ulivyotenda, uliyekidharau kiapo kwa kulivunja agano. Walakini nitalikumbuka agano langu nililolifanya pamoja nawe, katika siku za ujana wako, nami nitaweka imara agano la milele pamoja nawe. Hapo ndipo utakapozikumbuka njia zako, na kutahayarika, hapo utakapowakaribisha maumbu yako, walio wakubwa wako na wadogo wako; nami nitakupa hao wawe binti zako, lakini si kwa agano lako. Nami nitaweka imara agano langu nawe; nawe utajua ya kuwa mimi ndimi Bwana; upate kukumbuka, na kufadhaika, usifumbue kinywa chako tena, kwa sababu ya aiba yako; hapo nitakapokusamehe yote uliyoyatenda, asema Bwana Mungu. |
Wimbo wa Katikati. Isa 12:2-6
1. Tazama, Mungu ndiye wokovu wangu; Nitatumaini wala sitaogopa; Maana Bwana Yehova ni nguvu zangu na wimbo wangu; naye amekuwa wokovu wangu.
(K) Hasira yako imegeukia mbali, nawe unanifariji moyo. 2. Basi, kwa furaha mtateka maji Katika visima vya wokovu. Na katika siku hiyo mtasema, Mshukuruni Bwana, liitieni jina lake; Litajeni jina lake kuwa limetukuka. (K) 3. Mwimbieni Bwana; kwa kuwa ametenda makuu; Na yajulikane haya katika dunia yote. Paza sauti, piga kelele, mwenyeji wa Sayuni; Maana Mtakatifu wa Israeli ni mkuu kati yako. (K) |
Injili. Mt 19:3-12
Mafarisayo walimwendea Yesu wakamjaribu, wakimwambia, “Je, Ni halali mtu kumwacha mkewe kwa kila sababu?” Akajibu, akawaambia, “Hamkusoma ya kwamba yeye aliyewaumba mwanzo, aliwaumba mtu mume na mtu mke, akasema, ‘Kwa sababu hiyo, mtu atamwacha babaye na mamaye, ataambatana na mkewe; na hao wawili watakuwa mwili mmoja? Hata wamekuwa si wawili tena, bali mwili mmoja. Basi aliowaunganisha Mungu, mwanadamu asiwatenganishe. Wakamwambia, Jinsi gani basi Musa aliamuru kumpa hati ya talaka, na kumwacha?” Akawaambia, Musa, kwa sababu ya ugumu wa mioyo yenu, aliwapa ruhusa kuwaacha wake zenu; lakini tangu mwanzo haikuwa hivi. Nami nawaambia ninyi, “Kila mtu atakayemwacha mkewe, isipokuwa ni kwa sababu ya uasherati, akaoa mwingine, azini; naye amwoaye yule aliyeachwa azini”. Wanafunzi wake wakamwambia, “Mambo ya mtu na mkewe yakiwa hivyo, haifai kuoa.” Lakini yeye akawaambia, “Si wote wawezao kulipokea neno hili, ila wale waliojaliwa. Maana wako matowashi waliozaliwa hali hiyo toka matumboni mwa mama zao; tena wako matowashi waliofanywa na watu kuwa matowashi; tena wako matowashi waliojifanya kuwa matowashi kwa ajili ya Ufalme wa Mbinguni. Awezaye kulipokea neno hili, na alipokee. |
TAFAKARI
UAMINIFU KATIKA MAAGANO: Kwa unabii wa Ezekiel, Mungu anaongea nasi kuhusu uasi wa mwanadamu dhidi ya mapendo yake kwetu. Ni kisa chenye simanzi kubwa, jinsi tulivyo wanyonge, na kutelekezwa bila misaada na mifumo ya kijamii mfano wa kichanga kilichotupwa bila nguo, wala hifadhi yoyote. Kwa huruma na wema wake Mungu hutupatia kila aina ya misaada tunayohitaji, afya njema, ajira, madaraka, marafiki na vitu vingi. Ila mara nyingi mapendo na shukrani hatumrudishii Yeye ila twajitapanya kwa wale tunaodhani kuwa marafiki zetu; ambao hawakuwa na muda nasi tulipokuwa duni. Tuwe na shukrani na waaminifu kwa mapendo ya Mungu kwetu. Katika injili, Bwana wetu Yesu Kristo anatukumbusha mpango wa Mungu katika maagano ya ndoa, kwamba ni agano la kudumu. Kwa kauli hii ya Bwana wetu Yesu Kristo anawaalika wanandoa wajitathimini kuhusu uaminifu katika maagano yao. Aidha, sote tunaalikwa tukijitathmini pia jinsi tunavyoishi uaminifu katika viapo mbalimbali tulivyofanya tukimtaja Mungu katika Ubatizo, Kipaimara na maisha wito wa kila mmoja wetu.
Sala: Ee Mungu utujalie tudumu katika maagano yetu ya kikristo. |