Somo 1. Yer 31:1-7
“Wakati huo, asema Bwana, nitakuwa Mungu wa jamaa zote za Israeli, nao watakuwa watu wangu.” Bwana asema hivi, “Watu wale walioachwa na upanga walipata neema jangwani; yaani, Israeli, hapo nilipokwenda kumstarehesha.” Bwana alinitokea zamani, akisema, “Naam, nimekupenda kwa upendo wa milele, ndiyo maana nimekuvuta kwa fadhili zangu. Mara ya pili nitakujenga, nawe utajengwa, Ee bikira wa Israeli, mara ya pili utapambwa kwa matari yako, nawe utatokea katika michezo yao wanaofurahi. Mara ya pili utapanda mizabibu juu ya milima ya Samaria; wapanzi watapanda, nao watayafurahia matunda yake. Maana kutakuwa siku moja, ambayo walinzi watalia juu ya vilima vya Efraimu, ‘Inukeni, tukaende Sayuni, kwa Bwana, Mungu wetu.’” Maana Bwana asema hivi, mwimbieni Yakobo kwa furaha, mkampigie kelele mkuu wa mataifa, tangazeni, sifuni, mkaseme, Ee Bwana, uwaokoe watu wako mabaki ya Israeli. |
Wimbo wa Katikati. Yer 31:10-131
1. Lisikieni neno la Bwana, (K) Bwana atatulinda kama mchungaji alindavyo kundi lake. 2. Nao watakuja, na kuimba katika mlima Sayuni, 3. Ndipo bikira atafurahi katika kucheza, |
Injili. Mt 15:21-28
Yesu aliondoka Genezareti akaenda kando pande za Tiro na Sidoni. Na tazama, mwanamke Mkananayo wa mipaka ile akatokea, akampazia sauti akisema, “Unirehemu, Bwana, Mwana wa Daudi; binti yangu amepagawa sana na pepo.” Wala yeye hakumjibu neno. Nao wanafunzi wake wakamwendea, wakamwomba, wakisema, “Mwache aende zake; kwa maana anapiga kelele nyuma yetu.” Akajibu, akasema, “Sikutumwa ila kwa kondoo waliopotea wa nyumba ya Israeli.” Naye akaja akamsujudia, akisema, “Bwana unisaidie. Akajibu, akasema, Si vema kukitwaa chakula cha wototo na kuwatupia mbwa.” Akasema, “Ndiyo, Bwana, lakini hata mbwa hula makombo yaangukayo mezani pa bwana zao.” Ndipo Yesu akajibu, akamwambia, “Mama, imani yako ni kubwa; na iwe kwako kama utakavyo.” Akapona binti yake tangu saa ile. |
TAFAKARI
UPENDO WA MUNGU NI WA MILELE, UNATUFANYA WAPYA: Unabii wa Yeremia katika somo la leo, ni mwaliko wa kutambua na kulipokea pendo la Mungu. Tunapokosa mahusiano mema na Mungu tukaenda mbali na pendo lake, maisha huwa ya shida na taabu, kwani hatuna ulinzi wa uhakika. Leo, tunaalikwa kama Israeli mteule wa Mungu kupokea unabii huo uliojaa upendo, ili tukajengeke upya, tuwe wapya katika imani, mahusiano, na hata shughuli tulizoshindwa kukamilisha kutokana na mafarakano zikamalizike kwa Baraka za Mungu ili nasi tuweze kusema, “Bwana uwaokoe watu wako.” Injili inaweka mbele yetu nguvu ya pendo la Mungu linalofanya yote kuwa mapya. Kupokea ukamilifu wa pendo la Mungu imani thabiti inatakiwa. Sisi nasi tunayo mahitaji ya kumwambia Yesu. Ni kwa njia imani twaweza kustahilishwa maombi yetu. Tuzingatie anachosema Yesu: Imani yako ni kubwa; na iwe kwako kama utakavyo.” SALA: Ee Bwana utujalie paji la imani. |