Somo 1. Isa 10:5-7, 13-16
Bwana asema hivi: Ole wake Ashuru! Fimbo ya hasira yangu, ambaye gongo lililo mkononi mwake ni ghadhabu yangu! Nitamtuma juu ya taifa lenye kukufuru, nitampa maagizo juu ya watu wa ghadhabu yangu, ateke nyara, na kuchukua mateka, na kuwakanyaga kama matope ya njiani. Lakini hivyo sivyo akusudiavyo mwenyewe, wala sivyo moyo wake uwazavyo; maana katika moyo wake akusudia kuharibu, na kukatilia mbali mataifa, wala si mataifa machache. Kwa maana amesema, kwa nguvu za mkono wangu nimetenda jambo hili, na kwa hekima yangu; maana mimi nina busara; nami nimeiondoa mipaka ya watu, nikaziteka akiba zao, nikawaangusha waketio juu ya viti vya enzi kama afanyavyo shujaa. Na mkono wangu umezitoa mali za mataifa kama katika kioto cha ndege; na kama vile watu wakusanyavyo mayai yaliyoachwa, ndivyo nilivyokusanya dunia yote; wala hapana aliyetikisa bawa, wala kufumbua kinywa, wala kulia. Je! Shoka lijisifu juu yake alitumiaye? Je! Msumeno ujitukuze juu yake auvutaye? Ingekuwa kana kwamba bakora ingewatikisa waiinuao, au fimbo ingemwinua yeye ambaye si mti. Kwa hiyo Bwana, Bwana wa majeshi, atawapelekea kukonda watu wake walionona; na badala ya utukufu wake kutawashwa kuteketea kama kuteketea kwa moto. |
Zab 94:5-10, 14-15
1. Ee Bwana wanawaseta watu wako; (K) Bwana hatawatupa watu wake. 2. Nao husema Bwana haoni; 3. Aliyelitia sikio mahali pake asisikie? 4. Kwa kuwa Bwana hatawatupa watu wake. |
Injili. Mt 11:25-27
Wakati ule Yesu alijibu akasema, Nakushukuru, Baba, Bwana wa mbingu na nchi, kwa kuwa mambo haya uliwaficha wenye hekima na akili, ukawafunulia watoto wachanga. Naam, Baba, kwa kuwa ndivyo ilivyopendeza mbele zako. Akasema, Nimekabidhiwa vyote na baba yangu; wala hakuna amjuaye Mwana, ila Baba; wala hakuna amjuaye Baba, ila Mwana, na yeyote ambaye Mwana apenda kumfunulia. |
TAFAKARI.
HEKIMA YA MUNGU: Nabii Isaya anaiashiria Asiria kama shoka mkononi mwa mtumiaji, mtumiaji wa Asiria ni Mungu. Ndiye aliyeiinua kama mwenye shamba anavyoliinua chipukizi katika shamba lake. Mungu anaitumia Asiria kuisafisha Yuda, mfano wa Wasiria unatumika kwa Wayuda ili wafanye toba. Wakati huu Asiria ikawa na majivuno ikidhani imekuwa na uweza na mafanikio. Hili lilimpelekea nabii Isaya kuikumbusha Asiria nafasi yake, akiwaambia, bila uweza wa mikono ya mtumia shoka, shoka halina kazi. Ilikuwa bure kwa Asiria kujivunia uweza na ushindi wake, bila kumpa Mungu nafasi. Ilipaswa ijinyenyekeshe mbele ya Mungu. Unyenyekevu unahimizwa na Kristo katika sehemu ya Injili ya leo. Waliofichwa wenye hekima na akili ya kiulimwenguni tofauti na watoto wachanga wanaobakia wanyoofu, wanyenyekevu na tayari kutii maelekezo. Waisraeli walialikwa kuitambua Hekima ya Mungu muda wote. Hekima ya Mungu ndiyo iliyotumika kumtuma Nabii Isaya awaonye na kuwaalika kufanya toba. Sala: Ee Bwana neema yako ituwezesha kuendelea kutambua hekima yako, kuipokea na kuiishi. |