Somo 1. Amo 7: 10-17
Amazia kuhani wa Betheli, alipeleka habari kwa Yeroboamu, mfalme wa Israeli, akisema,”Amosi amefanya fitina juu yako kati ya nyumba ya Israeli; nchi haiwezi kustahimili maneno yake yote. Kwa maana Amosi asema hivi,’Yeroboamu atakufa kwa upanga, na bila shaka Israeli atachukuliwa mbali, hali ya kufungwa, atoke katika nchi yake.’Tena Amazia akamwambia Amosi,”Ewe mwona, nenda zako,ikimbilie nchi ya Yuda, ukale mkate huko,ukatabiri huko; lakini usitabiri tena huku Betheli; kwa maana ni mahali patakatifu pa mfalme,nayo ni nyumba ya kifalme.”Ndipo Amosi akajibu akamwambia Amazia,”Mimi sikuwa nabii,wala sikuwa mwana wa nabii;bali nalikuwa mchungaji na mtunza mikuyu;naye Bwana akanitwaa, katika kufuatana na kundi; Bwana akaniambia,’Enenda uwatabirie watu wangu Israeli’. Basi, sasa lisikie neno la Bwana; Wewe unasema,’Usitabiri juu ya Israeli, wala usitoe neno lako juu ya nyumba ya Isaka.’Kwa hiyo, Bwana asema hivi,’Mke wako atakuwa kahaba mjini, na wana wako na binti zako wataanguka kwa upanga, na shamba lako litagawanywa kwa kamba, na wewe nwenyewe utakufa katika nchi iliyo najisi; na bila shaka Israeli atachukuliwa mbali hali ya kufungwa kutoka nchi yake.’ |
Wimbo wa Katikati. Zab 19:8-11
1. Ushuhuda wa Bwana ni amini, (K) Hukumu za Bwana ni kweli, na ni za haki kabisa. 2. Amri ya Bwana ni safi, 3. Hukumu za Bwana ni kweli, |
Injili. Mt 9:1-8
Yesu alipanda chomboni, akavuka, akafika mjini kwao. Na tazama, wakamletea mtu mwenye kupooza, amelala kitandani; naye Yesu, alipoiona imani yao, alimwambia yule mwenye kupooza, “Jipe moyo mkuu, mwanangu; umesamehewa dhambi zako. Na tazama, baadhi ya waandishi wakasema nafsini mwao, “Huyu anakufuru.” Naye Yesu hali akijua mawazo yao, akasema, “Mbona mnawaza maovu mioyoni mwenu?” Kwa maana rahisi ni lipi, ni kusema, Umesamehewa dhambi zako, au ni kusema, Ondoka, uende? Lakini mpate kujua ya kwamba Mwana wa Adamu anayo amri duniani ya kusamehe dhambi, akamwambia yule mwenye kupooza” Ondoka, ujitwike kitanda chako, uende nyumbani kwako.” Akaondoka, akaenda zake nyumbani kwake. Makutano walipomwona, walishikwa na hofu, wakamtukuza Mungu, aliyewapa watu amri ya namna hii. |
TAFAKARI.
HOFU TAKATIFU: Neno hofu linachukuliwa kwa maana mbili; ya kwanza ni hofu takatifu ambayo ni hofu juu ya Mungu, ni kujisikia uchaji na heshima kwake na kutii amri zake. Maana ya pili ni kuhofia jambo, wanyama au mtu, hatari za kimwili, maumivu, na uovu ni kuwa na woga na mambo ya jinsi hiyo na kuyaogopa. Kwenye Injili ya leo wale makutano walipomwona Kristo walishikwa na hofu, wakamtukuza Mungu. Hii ndiyo hofu takatifu ambayo ni kumcha Bwana, ni hofu juu ya mambo matakatifu, inatokea mara kwa mara mtu anapokutana na jambo la heshima na analostahili kulipatia heshima. Maandiko matakatifu yanatufundisha “Asili ya Hekima ni kumcha Bwana, (Mithali 9:10, Zaburi 111: 10).” Tukitazama ujumbe wa somo la kwanza tunakutana na nabii anayefikisha ujumbe wa Mungu kwa watu hawaupokei ikiwa ni pamoja na Amazia kuhani wa kiyahudi kumfukuza nabii kutoka katika ufalme wa Kaskazini. Tunajifunza katika ujumbe wa neno la Mungu tusiwe kama watu wa Israeli wakiongozwa na Amazia walioukataa ujumbe wa Neno la Mungu bali tuige mfano mzuri wa kumcha Mungu. |