Somo 1. 1 Fal 18:20-39
Ahabu alipeleka watu kwa wana wa Israeli wote, akawakusanya manabii pamoja katika mlima wa Karmeli. Naye Eliya akawakaribia watu wote, akanena, Mtasita-sita katikati ya mawazo mawili hata lini? Bwana akiwa ndiye Mungu, mfuateni; bali ikiwa Baali ni Mungu, haya! Mfuateni yeye. Wale watu hawakumjibu neno. Ndipo Eliya akawaambia watu, Mimi nimesalia, mimi peke yangu, nabii wa Bwana; lakini manabii wa Baali ni watu mia nne na hamsini. Kwa hiyo na watutolee ng’ombe wawili; wao na wajichagulie ng’ombe mmoja, wamkatekate na kumweka juu ya kuni, wasitie moto chini; nami nitamtengeza huyo ng’ombe wa pili, na kumweka juu ya kuni, wala sitatia moto chini. Nanyi ombeni kwa jina la mungu wenu, nami nitaomba kwa jina la Bwana; na Mungu yule ajibuye kwa moto, na awe ndiye Mungu. Watu wote wakajibu wakasema, maneno haya ni mazuri. Eliya akawaambia manabii wa Baali, Jichagulieni ng’ombe mmoja, mkamtengeneze kwanza; maana ninyi ndio wengi; mkaliitie jina la mungu wenu, wala msitie moto chini. Wakamtwaa yule ng’ombe waliyepewa, wakamtengeneza, wakaliitia jina la Baali tangu asubuhi hata adhuhuri, wakisema, Ee Baali, utusikie. Lakini hapakuwa na sauti, wala aliyejibu. Nao wakaruka-ruka juu ya madhabahu waliyoifanya. Ikawa, wakati wa adhuhuri, Eliya akawafanyia dhihaka, akasema, Mwiteni kwa sauti kuu; maana ni mungu huyo; labda anazungumza, au ana shughuli, au anasafiri, au labda amelala, sharti aamshwe. Wakapiga kelele wakajikata-kata kwa visu na nyembe kama ilivyo desturi yao, hata damu ikawachuruzika. Ikawa, wakati wa adhuhuri ulipopita, walitabiri hata wakati wa kutoa dhabihu ya jioni; lakini hapakuwa na sauti, wala aliyejibu, wala aliyeangalia. Kisha Eliya akawaambia watu wote, nikaribieni mimi. Watu wote wakamkaribia. Akaitengeneza madhabahu ya Bwana iliyovunjika. Eliya akatwaa mawe kumi na mawili, kwa hesabu ya kabila za wana wa Yakobo, aliyejiliwa na neno la Bwana na kuambiwa, jina lako litakuwa Israeli. Naye akaijenga madhabahu ya Bwana kwa mawe hayo katika jina la Bwana; akafanya mfereji, kama wa vipimo viwili vya mbegu, ukiizunguka madhabahu. Kisha akazipanga zile kuni, akamkata yule ng’ombe vipande vipande, akaviweka juu ya kuni. Akasema, jazeni mapipa manne maji, mkayamwage juu ya sadaka ya kuteketezwa, na juu ya kuni. Akasema, fanyeni mara ya pili. Wakafanya mara ya pili. Akasema, fanyeni mara ya tatu. Wakafanya mara ya tatu. Yale maji yakaizunguka madhabahu; akaujaza mfereji maji. Ikawa, wakati wa kutoa dhabihu ya jioni, Eliya nabii akakaribia, akasema, Ee Bwana, Mungu wa Ibrahimu, na wa Isaka, na wa Israeli, na ijulikane leo ya kuwa wewe ndiwe Mungu katika Israeli, na ya kuwa mimi ni mtumishi wako, na ya kuwa nimefanya mambo haya yote kwa neno lako. Unisikie, Ee Bwana, unisikie, ili watu hawa wajue ya kuwa wewe, Bwana, ndiwe Mungu na ya kuwa wewe umewageuza moyo wakurudie. Ndipo moto wa Bwana ukashuka, ukaiteketeza sadaka ya kuteketezwa, na kuni, na mawe, na mavumbi, ukayaramba yale maji yaliyokuwamo katika mfereji. Na watu wote walipoona, wakaanguka kifudifudi wakasema, Bwana ndiye Mungu, Bwana ndiye Mungu. |
Wimbo wa Katikati. Zab 16:1-2, 4-5, 8, 11
1. Mungu, unihifadhi mimi, (K) Mungu, unihifadhi mimi, kwa maana nakukimbilia Wewe. 2. Huzuni zao zitaongezeka 3. Bwana ndiye fungu la posho langu, 4. Utanijulisha njia ya uzima |
Injili. Mt 5:17-19
Yesu aliwaambia wanafunzi wake: Msidhani ya kuwa nalikuja kutangua torati au manabii; la, sikuja kutangua, bali kutimiliza. Kwa maana, amin, nawaambia, Mpaka mbingu na nchi zitakapoondoka, yodi moja wala nukta moja ya torati haitaondoka, hata yote yatimie. Basi mtu ye yote atakayevunja amri moja katika hizi zilizo ndogo, na kuwafundisha watu hivyo, ataitwa mdogo kabisa katika ufalme wa mbinguni; bali mtu atakayezitenda na kuzifundisha, huyo ataitwa mkubwa katika ufalme wa mbinguni. |
TAFAKARI
TUISHI KWA KADIRI YA SHERIA ZA MUNGU: Katika Injili ya leo Yesu anatufundisha namna nzuri ya kuishi sheria za Mungu ili kufikia malengo ya sheria hizo. Sheria za Mungu hazipingani na sheria nzuri za kijamii kwani zote zina nafasi ya pekee katika maisha yetu. Tunahitaji kutambua uwiano wa sheria hizo na kutenda kwa kufuata utaratibu uliowekwa. Ujio wa Kristo hauondoi utaratibu mzuri wa Agano la Kale bali kwa njia ya Kristo tunapata ukamilifu wa taratibu hizo. Kitendo cha Yesu kusema hakuja kutengua sheria bali kukamilisha ni ashirio kuwa Mkristo hapaswi kutumia kigezo cha Imani ili kupinga taratibu nzuri za kijamii. Badala ya kuonesha upinzani kwa sheria za Mungu na sheria za kijamii tuangalie manufaa yatokanayo na sheria hizo na tulenge kuzitekeleza kwa upendo, kwani sheria zote zinahitimishwa na sheria moja ya upendo kwa Mungu na jirani. Tuwaombee wanaotunga sheria na kuzisimamia wafanye hivyo kwa manufaa ya taifa lote la Mungu. Sala: Ee Mungu nijalie moyo wa kuzingatia sheria zako. |