Somo 1. 1 Fal 21:17-29
Neno la Bwana likamjia Eliya Mtishbi, kusema, “Ondoka, ushuke ukutane na Ahabu mfalme wa Israeli, akaaye katika Samaria; yuko katika shamba la mizabibu la Nabothi, ndiko alikoshukia ili alitamalaki. Ukamwambie, ukisema, ‘Bwana asema hivi, Je! Umeua, ukatamalaki?’ Nawe utamwambia, kusema, ‘Bwana asema hivi: Mahali pale mbwa walipoiramba damu ya Nabothi, mbwa watairamba na damu yako, naam, damu yako’.” Ahabu akamwambia Eliya, “Je! Umenipata, ewe adui yangu?” Akamwambia, “Nimekupata, kwa sababu umejiuza utende yaliyo mabaya machoni pa Bwana. Angalia, nitaleta mabaya juu yako; nami nitakuangamiza kabisa, nitamkatia Ahabu kila mume, aliyefungwa na aliyeachwa katika Israeli. Kisha nitaifanya nyumba yako iwe kama nyumba ya Yeroboamu mwana wa Nebati, na kama nyumba ya Baasha mwana wa Ahiya, kwa ajili ya chukizo ulilonichukiza, hata kunighadhibisha, ukawakosesha Israeli. Tena Bwana alinena habari za Yezebeli, akisema, Mbwa watamla Yezebeli katika kiwanja za Yezreeli. Mtu wa nyumba ya Ahabu afaye mjini, mbwa watamla, na yeye afaye mashamba ndege wa angani watamla.” Lakini hapakuwa na mtu kama Ahabu, aliyejiuza atende maovu machoni pa Bwana, ambaye Yezebeli mkewe alimchochea. Akachukiza mno, kwa kuzifuata sanamu sawasawa na yote waliyoyafanya Waamori, Bwana aliowafukuza mbele ya wana wa Israeli. Ikawa, Ahabu alipoyasikia maneno hayo, akayararua mavazi yake, akavaa magunia mwilini mwake, akafunga, akajilaza juu ya magunia, akaenda kwa upole. Neno la Bwana likaja kwa Eliya Mtishbi, kusema, “Huoni jinsi Ahabu alivyojidhili mbele yangu? Basi kwa sababu amejidhili mbele yangu, sitayaleta yale mabaya katika siku zake; ila katika siku za mwanawe nitayaleta mabaya hayo juu ya nyumba yake.” |
Wimbo wa Katikati. Zab 51:3-6, 11, 16
“1. Ee Mungu unirhemu, sawasawa na Fadhili zako.
Kiasi cha wimgi wa rehema zako,
Uyafute maksa yangu.
Unitakase dhambi zangu.
(K) Ee Mungu uturehemu uyafute makosa yetu.
2. Maana nimejua mimi makossa yangu,
Na dhambi yangu I mbele yangu daima.
Nimekutenda dhambi Wewe peke yako. (K)
3. Usitiri uso wako usitazame dhambi zangu,
Uzifute hatia zangu zote.
Ee Bwana, uifumbue modomo yangu,
Na kinywa change kitazinena sifa zako. (K)”
Injili. Mt 5:43-48
Yesu aliwaambia wanafunzi wake: “Mmesikia kwamba imenenwa, Umpende jirani yako, na, Umchukie adui yako; lakini mimi nawaambia, Wapendeni adui zenu, waombeeni wanaowaudhi; ili mpate kuwa wana wa Baba yenu aliye mbinguni; maana yeye huwaangazia jua lake waovu na wema, huwanyeshea mvua wenye haki na wasio haki. Maana mkiwapenda wanaowapenda ninyi, mwapata thawabu gani? Hata watoza ushuru; je! Nao hawafanyi yayo hayo? Tena mkiwaamkia ndugu zenu tu, mnatenda tendo gani la ziada? Hata watu wa mataifa, je! nao hawafanyi kama hayo? Basi ninyi mtakuwa wakamilifu, kama Baba yenu wa mbinguni alivyo mkamilifu. |
TAFAKARI
KUISHI UTAKATIFU: Leo Yesu anatupa mwaliko wa kuishi utakatifu. Ukristo unatutaka tuishi kinyume na mtazamo wa walimwengu. Katika hali ya kawaida adui si rafiki na anapaswa kuchukiwa na kutengwa mbali kabisa. Leo Yesu anatufundisha ili kufikia utakatifu ni lazima kutenda tofauti na mtazamo huu wa walimwengu. Sote tumeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu hivyo tunapaswa kupendana. Ile amri ya kale ya kumpenda jirani na kumchukia adui haina nafasi tena. Yesu ameitengua na kututaka tuoneshe upendo kwa watu wote. Yesu aliweka fundisho hili katika matendo kwani alipokuwa anakata roho pale msalabani aliwaombea maadui zake ambao walimtesa na kusababisha kifo chake. Yesu anatutaka tuishi hivyo ili tufikie utakatifu na hili linawezekana kwa kubadili namna yetu ya kufikiri kibinadamu. Upendo wa kweli hautegemei manufaa yatokanayo na upendo huo. Upendo wa kweli unakusudia mema kwa wengine bila kutafuta maslahi binafsi. Hivi ndivyo Yesu alivyotupenda nasi tunapaswa kupendana hivyo. SALA: Ee Yesu utusaidie kushinda chuki na kisasi. |