Muziki-TV-728x90

Masomo ya misa

Masomo ya Misa Juni 6

By

on

Tumsifu Yesu Kristo. Karibu Katika Masomo ya Misa 06/06/2024

2024 JUNI 6 : ALHAMISI-JUMA LA 9 LA MWAKA

Mt. Norberti, Askofu
Rangi: Kijani
Zaburi: Juma 4

Somo 1. 2 Tim 2:8-15

Mkumbuke Yesu Kristo, aliyefufuka katika wafu, wa uzao wa Daudi kama inenavyo injili yangu. Nami katika hiyo nimeteswa hata kufungwa kama mtenda mabaya; lakini neno la Mungu halifungwi! Kwa ajili ya hilo nastahimili mambo yote, kwa ajili ya wateule, ili wao nao waupate wokovu ule ulio katika Kristo Yesu, pamoja na utukufu wa milele. Ni neno la kuaminiwa. Kwa maana, kama tukifa pamoja naye, tutaishi pamoja naye pia; kama tukistahimili, tutamiliki pamopja naye; kama tukimkana yeye, yeye naye atatukana sisi; kama sisi hatuamini, yeye hudumu kwa kuaminiwa. Kwa maana hawezi kujikana mwenyewe. Uwakumbushe mambo hayo, ukiwaonya machoni pa Mungu, wasiwe na mashindano ya maneno, ambayo hayana faida, bali huwaharibu wasikiao. Jitahidi kujionyesha kuwa umekubaliwa na Mungu, mtenda kazi asiye na sababu ya kutahayari, ukitumia kwa halali neno la kweli.

Wimbo wa Katikati. Zab 25:4-5, 8-10, 14

1. Ee Bwana, unijulishe njia zako,
Unifundishe mapito yako,
Uniongoze katika kweli yako,
Na kunifundisha.

(K) Ee Bwana, unijulishe njia zako.

2. Maana wewe ndiwe Mungu wa wokovu wangu,
Nakungoja wewe mchana kutwa.
Kwa hiyo atawafundisha wenye dhambi njia.
Wenye upole atawaongoza katika hukumu,
Wenye upole atawafundisha njia yake. (K)

3. Njia zote za Bwana ni Fadhili na kweli,
Kwao walishikao agano lake na shuhuda zake.
Siri ya Bwana iko kwao wamchao,
Naye atawajulisha agano lake. (K)

Injili. Mk 12:28-34

Mmoja wa waandishi alifika kwa Yesu akamwuliza, “Katika amri zote ni ipi iliyo ya kwanza?”  Yesu akamjibu, “Ya kwanza ndiyo hii, Sikia, Israeli, Bwana Mungu wetu ni Bwana mmoja. Nawe mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa akili zako zote, na kwa nguvu zako zote. Na ya pili ndiyo hii, Mpende jirani yako kama nafsi yako.  Hakuna amri nyingine iliyo kuu kuliko hizi.” Yule mwandishi akamwambia, “Hakika, Mwalimu, umesema vema ya kwamba Mungu ni mmoja, wala hakuna mwingine ila yeye; na kumpenda yeye kwa moyo wote, na kwa ufahamu wote, na kwa nguvu zote, na kumpenda jirani kama nafsi yako, kwafaa kuliko sadaka nzima za kuteketezwa na dhabihu zote pia.” Naye Yesu, alipoona kwamba amejibu kwa busara, alimwambia, “Wewe hu mbali na ufalme wa Mungu.” Wala hakuthubutu mtu kumsaili neno tena tokea hapo.

TAFAKARI

UPENDO KWA MUNGU NA KWA JIRANI: Upendo ni fadhila ya kimungu inayotuwezesha kumpenda Mungu kuliko viumbe vingine vyote na kuwapenda jirani zetu kama Yesu alivyotufundisha. Katika Injili ya leo tumesikia mwanasheria akitaka kujua ni amri ipi muhimu zaidi. Huyu ni tofauti na Masadukayo tuliowasikia jana. Zilikuwepo sheria nyingi sana hivyo alitaka kufahamu kupitia Yesu ajikite katika sheria ipi hasa katika zile nyingi. Jibu la Yesu ni kuwa sheria kubwa ni upendo kwa Mungu na jirani. Jibu la Yesu linatufundisha kuwa amri ya upendo kwa Mungu na jirani ni muhimu sana hata kuliko makongamano mbalimbali, mikesha mbalimbali, miugiza mbalimbali. Upendo kwa Mungu na jirani unatusaidia kuona mahitaji ya ndugu zetu na hivyo kuwasaidia ili kuwa na dini ya kweli kama tunavyofundishwa na Mtakatifu Yakobo anapoandika “Dini iliyo safi na isiyo na hitilafu mbele ya Mungu Baba ni hii: Kuwasaidia yatima na wajane katika shida zao, na kujilinda mwenyewe usichafuliwe na ulimwengu huu” Yak. 1:27.

Sala: Ee Mungu utujalie mapendo ya dhati.

About mzigotv

Recommended for you