Mzigo-TV-728x90

Masomo ya misa

Masomo ya Misa Agosti 1

By

on

Tumsifu Yesu Kristo. Karibu Katika Masomo ya Misa 01/08/2024

2024 AGOSTI 1: ALHAMISI-JUMA LA 17 LA MWAKA

Mt. Alphonsus Luguori
Rangi: Nyeupe

Zaburi: Juma 1

Somo 1. Yer 18:1-6

Neno hili ndilo lililomjia Yeremia, kutoka kwa Bwana, kusema, Ondoka, ukashuke mpaka nyumba ya mfinyanzi, na huko nitakusikizisha maneno yangu. Basi nikashuka mpaka nyumba ya mfinyanzi, na tazama, alikuwa akifanya kazi yake kwa magurudumu. Na chombo kile alichokuwa akikifinyanga, kilipoharibika mkononi mwake yule mfinyanzi, alikifanyiza tena kuwa chombo kingine, kama alivyoona vyema yule mfinyanzi kukifanya.  Ndipo neno la Bwana likanijia, kusema, Ee nyumba ya Israeli, je! Siwezi mimi kuwatendea ninyi vile vile kama mfinyanzi huyu alivyotenda? Asema Bwana. Angalieni, kama udongo ulivyo katika mkono wa mfinyanzi, ndivyo mlivyo katika mkono wangu, Ee nyumba ya Israeli.

Wimbo wa Katikati. Zab 146: 1-6

1. Ee nafsi yangu, umsifu Bwana, Nitamsifu Bwana muda nitakaoishi, Nitamwimbia Mungu ningali ni hai.

(K) Heri ambaye Mungu wa Yakobo ni msaada wake.

2. Msiwatumainie wakuu, Wala binadamu ambaye hakuna wokovu kwake. Pumzi yake hutoka, huurudia udongo wake, Siku hiyo mawazo yake yatapotea. (K)

3. Heri ambaye Mungu wa Yakobo ni msaada wake, na tumaini lake ni kwa Bwana, Mungu wake. Aliyezifanya mbingu nan chi, bahari na vitu vyote vinavyoonekana. (K)

Injili. Mt 13:47-53

Yesu aliwaambia wanafunzi wake: Ufalme wa mbinguni umefanana na juya, lililotupwa baharini, likakusanya wa kila namna; hata lilipojaa, walilivuta Pwani, wakaketi, wakakusanya walio wema vyomboni, bali walio wabaya wakawatupa. Ndivyo itakavyokuwa katika mwisho wa dunia; Malaika watatokea, watawatenga waovu mbali na wenye haki, na kuwatupa katika tanuru ya moto; ndiko kutakuwako kilio na kusaga meno. Yesu aliwauliza, Mmeyafahamu hayo yote? Wakamwambia, Naam. Akawaambia, kwa kwa sababu hiyo, kila mwandishi mwenye elimu ya ufalme wa mbinguni amefanana na mtu mwenye nyumba atoaye katika hazina yake vitu vipya na vya kale. Ikawa Yesu alipoimaliza mifano hiyo, alitoka akaenda zake.

TAFAKARI

KILA MMOJA ANA THAMANI MBELE YA MUNGU: Neno la Mungu linatuangaza kutambua udhaifu wetu na jinsi Mungu tunayemwamini kwa wema wake anavyoweza kutupatia hadhi mpya na kutufanya wenye thamani tena hata baada ya kutoroka katika mikono yake kwa njia zisizompendeza. Tunapopata neema ya kurudi kwake tunafanyika vyombo vipya na vyenye uzuri na thamani. Tukitambua ya kuwa tuna thamani sana kwake zaidi ya udongo wa mfinyanzi ulivyo wa thamani mikononi mwa mfinyanzi. Neno hili litutulize wote kutokana na misukosuko ya maisha tuliyopitia na tusiogope kurudi kwake atufinyange upya. Kwa somo la Injili ya leo, thamani yetu inaendeelea kudhihirishwa kwani kila mmoja anapewa nafasi ya kuhudumiwa na kanisa bila ubaguzi, kama juya linavyovuta wa kila aina linapotupwa baharini. Kanisa ni mvuvi, kwa njia ya mafundisho anapita baharini kwenye uharibifu ili kufanya uvuvi salama, kututafuta tulipo. 

SALA: Ee Mungu utustahilishe kuingia katika ufalme wako.

About mzigotv

Recommended for you