Mzigo-TV-728x90

Masomo ya misa

Masomo ya Misa Julai 1

By

on

Tumsifu Yesu Kristo. Karibu Katika Masomo ya Misa 01/07/2024

2024 JULAI 1: JUMATATU; JUMA  LA 13 LA MWAKA

Mt. Gallus, Askofu
Rangi: Kijani

Zaburi: 

Somo 1. Amo 2:6-10, 13-16

Haya ndiyo asemayo Bwana; kwa makosa matatu ya Israeli, naam, kwa manne, sitaizuia adhabu yake isimpate; kwa sababu wamewauza wenye haki kwa fedha, na maskini kwa jozi ya viatu; nao hutwetea mavumbi yaliyo juu ya vichwa vya maskini, na kuipotosha njia ya wenye upole; na mtu na baba yake humwendea mwanamke mmoja, hata kulitia unajisi jina langu takatifu; nao hujilaza karibu na kila madhabahu juu ya nguo zilizowekwa rehani, na katika nyumba ya Mungu wao hunywa divai ya watu waliotozwa fedha. Lakini nalimwangamiza mwamori mbele yao, ambaye urefu wake ulikuwa kama urefu wa mierezi, tena alikuwa na nguvu kama mialoni; lakini naliyaangamiza matunda yake toka juu, na mizizi yake toka chini. Pia naliwapandisha ninyi kutoka nchi ya Misri, nikawaongoza muda wa miaka arobaini jangwani, ili mpate kuimiliki nchi ya mwamori. Tazameni, nitawalemea ninyi, kama gari lilemeavyo lililojaa miganda. Naye apigaye mbio atapotewa na kimbilio; wala aliye hodari hataongeza nguvu zake; wala shujaa hatajiokoa nafsi yake; wala apindaye upinde hatasimama; wala aliye mwepesi wa miguu hataokoka; wala apandaye farasi hatajiokoa nafsi yake; naye mwenye moyo mkuu miongoni mwa mashujaa atakimbia uchi siku ile, asema Bwana.

Wimbo wa Katikati. Zab 50:16-23

1. Mtu asiye haki, Mungu amwambia,
Una nini wewe kuitangaza sheria yangu,
Na kuliweka agano langu kinywani mwako?
Maana wewe umechukia maonyo,
Na kuyatupa maneno yangu nyuma yako.

(K) Yafahamuni hayo, ninyi mnaomsahau Mungu.

2. Ulipomwona, mwivi ulikuwa radhi naye,
Ukashirikiana na wazinzi.
Umekiachia kinywa chako kinene mabaya,
Na ulimi wako watunga hila. (K)

3. Umekaa na kumsengenya ndugu yako,
Na mwana wa mama yako umemsingizia.
Ndiyo ulivyofanya, nami nikanyamaza;
Ukadhani ya kuwa Mimi ni kama wewe.
Walakini nitakukemea;
Nitayapanga hayo mbele ya macho yake. (K)

4. Yafahamuni hayo,
Ninyi mnaomsahau Mungu.
Nisije nikawararueni,
Asipatikane mwenye kuwaponya.
Atoaye dhabihu za kushukuru,
Ndiye anayenitukuza.
Naye autengenezaye mwenendo wake,
Nitamwonyesha wokovu wa Mungu. (K)  

Injili. Mt 8:18-22

Yesu alipoona makutano mengi wakimzunguka aliamuru kuvuka kwenda ng’ambo. Mwandishi mmoja akamwendea, akamwambia, Mwalimu, nitakufuata kokote uendako. Yesu akamwambia, mbweha wana pango, na ndege wa angani wana vioto; lakini Mwana wa Adamu hana pa kulaza kichwa chake. Mwingine katika wanafunzi wake akamwambia, Bwana, nipe ruhusa kwanza, niende nikamzike baba yangu. Lakini Yesu akamwambia, Nifuate; waache wafu wazike wafu wao.

TAFAKARI

GHARAMA YA KUMFUATA KRISTO: Mwanafunzi wa Kristo ni mtu anayekubali kuacha mambo mengine yote ili ajifunze kwa Kristo na kusaidia katika kueneza habari njema ya Yesu Kristo. Katika Injili mwandishi alitamani kuwa mfuasi wa Kristo, bila shaka hakujua gharama ya kuwa mfuasi wa Kristo. Kuwa mfuasi wa Kristo ni mchakato ambao mwanafunzi anastawi ndani ya Bwana Yesu Kristo na akisukumwa na Roho Mtakatifu, anayeishi ndani ya mioyo yao. Akichochewa kuondokana na shinikizo na majaribu ya maisha ya sasa na kuwa zaidi kama Kristo. Mwandishi anajulishwa kuwa ni pamoja na kujisalimisha jumla, kutofungwa na makandokando au masharti nje ya kumfuata Kristo. Kuna hadithi ya kijana mmoja aliyepata ufadhili wa kwenda kusoma masomo ya juu akakataa akisema, nitaenda nitakapokuwa nimemzika baba yangu, baba yake alikuwa na afya njema na alikuwa hajafikisha miaka hamsini. Tofauti yake, Amosi amekuwa makini kuitikia sauti ya Mungu iliyomwita kuwa nabii na kuwatetea wanyonge waliokuwa wengi waliokandamizwa na wachache katika Israeli.

Sala: Ee Bwana utuwezeshe kuitikia sauti yako pasipo ya kuwa na visingizio.

About mzigotv

Recommended for you