Somo 1. Hek 1: 13-15; 2:23-24
Mungu hakuifanyiza mauti, wala haimpendezi walio hai wakipotea. Kwa maana aliviumba vitu vyote ili vipate kuwako, na nguvu za uzazi zilizomo ulimwenguni ni za kuleta siha, wala hakuna ndani yake sumu yo yote ya uharibifu, wala ahera haina milki kama ya kifalme hapa duniani; Maana haki yaishi milele. Yaani, Mungu alimwumba mwanadamu ili apate kutokuharibika, kwa mfano wake mwenyewe, ila ulimwengu uliingiwa na mauti kwa husuda yake Shetani, nao walio wa upande wake hupata kuionja. |
Wimbo wa Katikati. Zab 30: 2-6, 11-13
1. Bwana nitakutukuza kwa maana umeniinua, (K) Ee Bwana, nitakutukuza kwa maana umeniinua. 2. Mwimbieni Bwana Zaburi, 3. Ee Bwana, usikie, unirehemu, |
Somo 2. 2 Kor 8: 7, 9, 13-15
Kama mlivyo na wingi wa mambo yote; imani, na usemi, na elimu, na bidii yote; na upendo wenu kwetu sisi; basi vivyo hivyo mpate wingi wa neema hii pia. Maana mmejua neema ya Bwana wetu Yesu Kristo, jinsi alivyokuwa maskini kwa ajili yenu, ingawa alikuwa tajiri, ili kwamba ninyi mpate kuwa matajiri kwa umaskini wake. Maana sisemi hayo, ili wengine wapate raha nanyi mpate dhiki; bali mambo yawe sawasawa; wakati huu wa sasa wingi wenu uwafae upungufu wao, ili na wingi wao uwafae ninyi mtakapopungukiwa; ili mambo yawe sawasawa. Kama ilivyoandikwa, aliyekusanya vingi, hakuzidi, wala yeye aliyekusanya vichache hakupungukiwa. |
Injili. Mk 5: 21-43
Yesu alipokwisha kuvuka kurudi ng’ambo katika kile chombo, wakamkusanyikia mkutano mkuu; naye alikuwa kando ya bahari. Akaja mtu mmoja katika wakuu wa sinagogi, jina lake Yairo; hata alipomwona, akaanguka miguuni pake, akimsihi sana, akisema, Binti yangu mdogo yu katika kufa; nakuomba uje, uweke mkono wako juu yake, apate kupona, na kuishi. Akaenda pamoja naye. Mkutano mkuu wakamfuata, wakimsongasonga. Na mwanamke mmoja mwenye kutoka damu muda wa miaka kumi na miwili, na kuteswa mengi kwa mikono ya matabibu wengi, amegharimiwa vitu vyote alivyo navyo, kusimfae hata kidogo, bali hali yake ilizidi kuwa mbaya; aliposikia habari za Yesu, alipita katika mkutano kwa nyuma, akaligusa vazi lake; maana alisema, Nikiyagusa mavazi yake tu, nitapona. Mara chemchemi ya damu yake ikakauka, naye akafahamu mwilini mwake kwamba amepona msiba ule. Mara Yesu, hali akifahamu nafsini mwake kwamba nguvu zimemtoka, akageuka kati ya mkutano, akasema, Ni nani aliyenigusa mavazi yangu? Wanafunzi wake wakamwambia, Je! wawaona makutano wanavyokusonga-songa, nawe wasema, Ni nani aliyenigusa? Akatazama pande zote ili amwone yule aliyelitenda neno hilo. Na yule mwanamke akaingiwa na hofu na kutetemeka, akijua lililompata, akaja akamwangukia, akamweleza kweli yote. Akamwambia, Binti, imani yako imekuponya, enenda zako kwa amani, uwe mzima, usiwe na msiba wako tena. Hata alipokuwa katika kunena, wakaja watu kutoka kwa yule mkuu wa sinagogi, wakisema, Binti yako amekwisha kufa; kwani kuzidi kumsumbua mwalimu? Lakini Yesu, alipolisikia lile neno likinenwa, akamwambia mkuu wa sinagogi, Usiogope, amini tu. Wala hakumruhusu mtu afuatane naye, ila Petro, na Yakobo, na Yohane nduguye Yakobo. Wakafika nyumbani kwa yule mkuu wa sinagogi, akaona ghasia, na watu wakilia, wakifanya maombolezo makuu. Alipokwisha kuingia, akawaambia, Mbona mnafanya ghasia na kulia? Kijana hakufa, bali amelala tu. Wakamcheka sana. Naye alipokwisha kuwatoa nje wote, akamtwaa babaye yule kijana na mamaye, na wale walio pamoja naye, akaingia ndani alimokuwamo yule kijana. Akamshika mkono kijana, akamwambia, Talitha, kumi; tafsiri yake, Msichana, nakuambia, Inuka. Mara akasimama yule kijana, akaenda; maana alikuwa amepata umri wa miaka kumi na miwili. Mara wakashangaa mshangao mkuu. Akawaonya sana, mtu asijue habari ile; akaamuru apewe chakula. |
TAFAKARI.
IMANI HUPONYA SALA: Ee Yesu uguse maisha yetu kwa Neno na Sakrementi zako. |