Tumsifu Yesu Kristo. Karibu Katika Masomo ya Misa 13/07/2024
2024 JULAI 13: JUMAMOSI-JUMA LA 14 LA MWAKA
Mt. Henri
Rangi: Kijani
Zaburi: Juma 2
Somo 1. Isa 6:1-8
Katika mwaka ule aliokufa mfalme Uzia nalimwona Bwana ameketi katika kiti cha enzi, kilicho juu sana na kuinuliwa sana, na pindo za vazi lake zikalijaza hekalu. Juu yake walisimama maserafi; kila mmoja alikuwa na mabawa sita; kwa mawili alifunika uso wake, na kwa mawili alifunika miguu yake, na kwa mawili aliruka. Wakaitana, kila mmoja na mwenzake, wakisema, “Mtakatifu, Mtakatifu, Mtakatifu, ni Bwana wa majeshi; dunia yote imejaa utukufu wake.” Na misingi ya vizingiti ikatikisika kwa sababu ya sauti yake aliyelia, nayo nyumba ikajaa moshi. Ndipo niliposema, “Ole wangu! Kwa maana nimepotea; kwa sababu mimi ni mtu mwenye midomo michafu; nami ninakaa kati ya watu wenye midomo michafu; na macho yangu yamemwona Mfalme, Bwana wa majeshi.” Kisha mmoja wa maserafi wale akaruka akanikaribia; naye alikuwa na kaa la moto mkononi mwake, ambalo alikuwa amelitwaa kwa makoleo toka juu ya madhabahu; akanigusa kinywa changu kwa kaa hilo, akaniambia, “Tazama, hili limekugusa midomo yako, na uovu wako umeondolewa, na dhambi yako imefunikwa.” Kisha nikaisikia sauti ya Bwana, akisema,” Nimtume nani, naye ni nani atakayekwenda kwa ajili yetu?” Ndipo niliposema,” Mimi hapa, nitume mimi!” |
Wimbo wa Katikati. Zab 93:1-2, 5
1.Bwana ametamalaki, amejivika adhama, (K) Bwana ametamalaki, amejivika adhama. 2.Naam, ulimwengu umethibitika usitikisike; Kiti chako kimekuwa thabiti tokea zamani; Wewe ndiwe uliye tangu milele. (K) 3.Shuhuda zako ni amini sana; |
Injili. Mt 10:24-33
Yesu aliwafundisha mitume wake: Mwanafunzi hampiti mwalimu wake, wala mtumwa hampiti bwana wake. Yamtosha mwanafunzi kuwa kama mwalimu wake, na mtumwa kuwa kama bwana wake. Ikiwa wamemwita mwenye nyumba Beelzebuli; je! Si zaidi wale walio wa nyumbani mwake? “Basi, msiwaogope, kwa maana hakuna neno lililositirika, ambalo halitafunuliwa; wala lililofichwa, ambalo halitajulikana. Niwaambialo ninyi katika giza, lisemeni katika nuru; na msikialo kwa siri, lihubirini juu ya nyumba. Msiwaogope wauuao mwili, wasiweze kuiua na roho; afadhali mwogopeni yule awezaye kuangamiza mwili na roho pia katika jehanum. Je! Mashomoro wawili hawauzwi kwa senti moja? Wala hata mmoja haanguki chini asipojua Baba yenu; lakini ninyi, hata nywele za vichwa vyenu zimehesabiwa zote. Msiogope basi; bora nyinyi kuliko mashomoro wengi. Basi, kila mtu atakayenikiri mbele ya watu, nami nitamkiri mbele za Baba yangu aliye mbinguni. Bali mtu ye yote atakayenikana mbele ya watu, nami nitamkana mbele za Baba yangu aliye mbinguni.” |
TAFAKARI.
TUENDELEE KUSHUHUDIA KWA UJASIRI: Siku moja mhubiri mashuhuri aliinuka kuhubiri akagundua kuwa kati ya aliokuwa akiwahubiria kulikuwa na mfalme wa Uajemi aliyekuwa mwovu sana, kuwa mahubiri yake yatamuumiza kwani atakapokuwa anaongea itakuwa kama anamshambulia. Kabla hajaanza kuhubiri alitafakari kidogo, halafu akajisemea kwa sauti kubwa; “Oh mhubiri, uwe makini na utakachokisema, mfalme wa Uajemi leo yupo hapa.” Halafu akatafakari tena halafu akasema, “Wewe mhubiri uwe makini nini ambacho hatokisema leo, Mfalme wa Wafalme yuko hapa leo.” Yesu aliongea dhidi ya uovu bila hofu yeyote. Anawaasa pia wanafunzi wake “Msiwaogope wauuao mwili, wasiweze kuiua na roho; afadhali mwogopeni yule awezaye kuangamiza mwili na roho pia katika jehanum.” Hakika Mungu pekee ndiye mwenye Mamlaka juu ya mwili na roho ya mwanadamu. Kwa kuelewa hilo nabii Isaya anarudia rudia katika unabii wake kuwa Mungu ni Mtakatifu. Isaya hakuacha kuukiri utakatifu wa Mungu mbele za watu na kwamba Mungu amewaita kuwa watakatifu. Sala: Ee Bwana utuwezeshe kupokea vema wito wa kuishi Utakatifu na kumsifu Mungu Mtakatifu. |