Mzigo-TV-728x90

Masomo ya misa

Masomo ya Misa Julai 14

By

on

Tumsifu Yesu Kristo. Karibu Katika Masomo ya Misa 14/07/2024

2024 JULAI 14: DOMINIKA YA 15 YA MWAKA

Rangi: Kijani
Zaburi: Tazama sala ya siku

Somo 1. Amo 7: 12-15

Amazia alimwambia Amosi, Ewe mwona, nenda zako, ikimbilie nchi ya Yuda, ukale mkate huko, ukatabiri huko; lakini usitabiri tena huku Betheli; kwa maana ni mahali patakatifu pa mfalme, nayo ni nyumba ya kifalme. Ndipo Amosi akajibu akamwambia Amazia, Mimi sikuwa nabii, wala sikuwa mwana wa nabii; bali nalikuwa mchungaji, na mtunza mikuyu; naye Bwana akanitwaa, katika kufuatana na kundi; Bwana akaniambia, Enenda uwatabirie watu wangu Israeli.

Wimbo wa Katikati. Zab 85: 9-14

1. Na nisikie atakavyosema Mungu Bwana,
Maana atawaambia watu wake amani,
Hakika wokovu wake u karibu na wamchao,
Utukufu ukae katika nchi yetu.

(K) Ee Bwana utuoneshe rehema zako utupe wokovu wako.

2. Fadhili na kweli zimekutana,
Haki na amani zimebusiana.
Kweli imechipuka katika nchi,
Haki imechungulia kutoka mbinguni. (K)

3. Naam, Bwana atatoa kilicho chema,
Na nchi yetu itatoa mazao yake.
Haki itakwenda mbele zake,
Nayo itazifanya hatua zake kuwa njia. (K)

Somo 2. Efe 1: 3-14

Atukuzwe Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, aliyetubariki kwa baraka zote za rohoni, katika ulimwengu wa roho, ndani yake Kristo; kama vile alivyotuchagua katika yeye kabla ya kuwekwa misingi ya ulimwengu, ili tuwe watakatifu, watu wasio na hatia mbele zake katika pendo. Kwa kuwa alitangulia kutuchagua, ili tufanywe wanawe kwa njia ya Yesu Kristo, sawasawa na uradhi wa mapenzi yake. Na usifiwe utukufu wa neema yake, ambayo ametuneemesha katika huyo Mpendwa. Katika yeye huyo, kwa damu yake, tunao ukombozi wetu, misamaha ya dhambi, sawasawa na wingi wa neema yake. Naye alituzidishia hiyo katika hekima yote na ujuzi; akiisha kutujulisha siri ya mapenzi yake, sawasawa na uradhi wake, alioukusudia katika yeye huyo. Yaani, kuleta madaraka ya wakati mkamilifu atavijumlisha vitu vyote katika Kristo, vitu vya mbinguni na vitu vya duniani pia. Naam, katika yeye huyo; na ndani yake sisi nasi tulifanywa urithi, huku tukichaguliwa tangu awali sawasawa na kusudi lake yeye, ambaye hufanya mambo yote kwa shauri la mapenzi yake. Nasi katika huyo tupate kuwa sifa ya utukufu wake, sisi tuliotangulia kumwekea Kristo tumaini letu. Nanyi pia katika huyo mmekwisha kulisikia neno la kweli, Habari Njema za wokovu wenu; tena mmekwisha kumwamini yeye, na kutiwa muhuri na Roho yule wa ahadi aliye Mtakatifu. Ndiye aliye arabuni ya urithi wetu, ili kuleta ukombozi wa milki yake, kuwa sifa ya utukufu wake.    

Injili. Mk 6: 7-13

Yesu aliwaita wale Thenashara, akaanza kuwatuma wawili wawili, akawapa amri juu ya pepo wachafu; akawakataza wasichukue kitu cha njiani isipokuwa fimbo tu; wala mkate, wala mkoba, wala pesa za bindoni; lakini wajifungie viatu, akasema, Msivae kanzu mbili. Akawaambia, mahali po pote mtakapoingia katika nyumba, kaeni humo hata mtakapotoka mahali pale. Na mahali po pote wasipowakaribisha ninyi wala kuwasikia, mtokapo huko, yakung’uteni mavumbi yaliyo chini ya miguu yenu, kuwa ushuhuda kwao. Wakatoka, wakahubiri kwamba watu watubu. Wakatoa pepo wengi, wakapaka mafuta watu wengi waliokuwa wagonjwa, wakawapoza. 

TAFAKARI

NENDA KATANGAZE NENO LA MUNGU
Neno utume linaashiria kutumwa. Hivyo katika utume kuna pande mbili: yupo anayetuma na anayetumwa. Yeye anayetuma anamtumia mtu mwingine ambaye anamtegemea kumfikishia vema ujumbe wake. Hivyo atampatia ujumbe huo kikamilifu na kumwezesha kwa nyenzo zote ili kuufikisha ujumbe wake. Anayetumwa anatumika kama chombo cha kuubeba ujumbe, anatumwa kuupeleka. Haitarajiwi hata mara moja kwa anayetumwa kuanza kuelezea mambo yake nje anayotumwa, vinginevyo ataisaliti kazi yake. Katika hali ya kawaida mmoja hawezi kujituma mwenyewe; ama atatuma mtu mwingine au atatekeleza mwenyewe na katika hilo la pili hauwi utume. Sisi wakristo tumetumwa kwenda kutangaza Neno la Mungu. Hili ndilo ambalo Kristo anatutaka na pia kutuwezesha: kutangaza habari njema ya wokovu na kuwafanya mataifa yote, yaani watu wote kumrudia Mungu na kuwa wanafunzi wake.
Utume wa kutangaza habari njema ni mwendelezo wa historia ya wokovu wa mwanadamu. Mwenyezi Mungu anatumia watu mbalimbali tangu zamani za mababu zetu ili kuufikisha ujumbe wake wa wokovu wa wanadamu. Ujumbe huu unawaendea wanadamu ambao wapo katika hali ya dhambi ili waokoke na kumrudia Mungu. “Utume wa Kristo na wa Roho Mtakatifu unakamilika katika Kanisa, utume huu wa pamoja unawahusisha waamini wa Kristo katika ushirika wake pamoja na Baba ndani ya Roho Mtakatifu: Roho hutayarisha watu, akiwaendea kwa neema yake ili kuwapeleka kwa Kristo.Anamdhihirisha kwao Bwana Mfufuka, anawakumbusha neno lake, anafumbua akili zao na kutambua kifo chake na ufufuko wake” (KKK 737).
Katika Injili ya Dominika hii tunamwona Kristo anawatuma wafuasi wake. Maudhui ya utume huo yanajionesha wazi: kuutangaza ufalme wa Mungu unafika kwetu kwa njia ya Kristo: kuhubiri toba, kuponya waliopagawa na pepo na kuwapaka mafuta. “Kanisa lasadiki katika uwepo unaohuisha, mganga wa roho na miili. Uwepo huu hutenda kazi kwa namna ya pekee kwa njia ya sakramenti, na kwa namna iliyo ya pekee kabisa kwa njia ya Ekaristi Takatifu, mkate uletao uzima wa milele, na ambao Mt. Paulo hudokeza uhusiano wake na afya ya mwili” (KKK 1509). Kristo anatuambia: “hiki ni chakula kishukacho kutoka mbinguni; si kama mababa walivyokula, wakafa; bali akilaye chakula hicho ataishi milele” (Yoh 6:58). Uhai na ufanisi wa utume wetu unafumbatwa katika fumbo la Ekaristi Takatifu ambalo ni ufunuo wa upendo wa Mungu na sababu ya umoja wa kikristo. Utume wetu wa kimisionari unatudai kuiishi Ekaristi Takatifu.
Chemchemi au chanzo cha utume wetu ni upendo wa Utatu Mtakatifu.Kutoka humo ndimo tunachota yale ambayo tunatumwa kwenda kuyatekeleza kwa ajili ya wokovu wa mwanadamu. Nje ya chanzo hicho hujikuta tunajitafutia vyanzo vya kidunia ambavyo hutupeleka katika kifo. Kutokana na hilo Kristo anatutaadharisha kutokuandamana na vitu vya kidunia: “msichukue kitu njiani…wala mkate…wala mkoba…wala fedha za kibindoni…msivae kanzu mbili.” Huu ni wito wa “ufukara wa kimisionari” ambao kwa sehemu kubwa leo hii unaathiriwa na upepo wa “biashara za kimisionari” “Biashara za kimisionari” hatari kubwa inayoiandama jumuiya ya waamini leo hii. Nguvu kubwa inaelekezwa sana katika kujiimarisha kiuchumi hata kama itaua utume halisi wa kutangaza habari njema na kuponya wagonjwa. Hatari hii kwa namna fulani huwa haionekani kwa urahisi na mwishoni tunaishia kuwapora watu fursa ya kuuona uso wa huruma ya Mungu.
Hili linaweza kudhihirishwa na namna ambavyo tunatumia nyenzo mbalimbali za kujipatia ridhiki kama vichaka vya kuwanyonya na kuwakandamiza watu wengine. Mara nyingi tunajidanganya na kujikita zaidi katika dhuluma ya utu wa mtu, kujitafutia mahitaji ya muhimu kama chakula, maji na afya. Sharti la Kristo ni moja: “msichukue kitu njiani”. Hii haimaanishi msile au msijipatie yaliyo muhimu. Katika ukarimu wa asili wa kibinadamu mmoja anapotoa huduma kwa hali ya upendo atapoka huduma muhimu kwa utumishi wake. Ndiyo maana Kristo anawaagiza akisema: “mahali popote mtakapoingia katika nyumba, kaeni humo hata mtakapotoka mahali pale.” Mmisionari anapaswa kujikabidhi katika ukarimu wa wenyeji wake. Ni agizo ambalo lilinuia kuwaepusha mitume kujihangaisha na kutafuta mahitaji ya kijamii kama chakula na malazi.
Na hivyo wito unatolewa kwa yeyote anayempokea mtume wa Mungu ambaye amefika kumtolea huduma kufanya ukarimu kwa kuwapatia mahitaji ya kawaida ya kibinadamu. Si rahisi kwa wananchi kukubali kuona tabibu wao anaishi maisha ya dhiki na njaa kubwa wakati wao wanacho chakula cha kutosha. Katika hali hiyo watampatia chakula kwa sababu kwa upande mwingine nao huitaji huduma yake. Kwa maneno mengine hapa tunaambiwa tuitangulize huduma ya kuustawisha kwanza ufalme wa Mungu na mengine tutapewa kwa ziada (rej. Lk 12:22 –41). Kristo anaongeza kuwa hata kwa wale wasiokuwa na ukarimu jibu lisiwe la vurugu na lawama bali kuwaachia ushuhuda wa uchoyo wao katika hali ya amani.
Mwarobaini wa kuepuka “umisionari wa kibiashara” na kuukumbatia “ufukara wa kimisionari” unapatikana katika undugu wa kikristo. Undugu wa kikristo unajikita katika udogo, kujikatalia, kujitolea katika huduma na nia ya kuwakumbatia watu wote wa Mungu hasa hasa walio fukara zaidi.” Hivyo aliwaasa watu wote hasa vijana “kuwa na uwezo wa kuzitambua sura mbalimbali ufukara katika jamii ya leo na kuwa ndugu kwa watu wote ambao wana hamu ya kukutana na Kristo.” Ulimwengu wa leo ambao unajidadavua katika mambo ya mali na vitu vya kuonekana; katika madaraka na sifa za kidunia ni kinzani kwa wito huu na matokeo yake ni kupindisha malengo ya utume tunaopewa na Kristo. Nguvu na ukuu wa mtu umejikita katika uwezo wa kifedha. Mambo haya yanatuadaa na kutufumba macho kiasi cha kutomwona Lazaro anayeteseka chini ya meza yangu ya chakula. Habari tunayoipeleka kwao si habari njema ya wokovu; huduma tunayowapatia si ya uponyaji. Tunageukia upepo wa kidunia wa nipe nikupe; tunakubaliana na msemo wa “mwenye nguvu mpishe.” Katika hali hii kwa hakika tunausaliti utume wetu. Sauti ya Kristo inaendelea kutuonya ikisema: “msichukue kitu njiani.”
Somo la kwanza linatufunulia upinzani wa ulimwengu katika kuupokea ujumbe wa Mungu. Amazia anaizuia sauti ya Mungu na hivyo kuendelea kubariki uovu wa mwanadamu ambao husambaratisha undugu. “Biashara za kimisionari” zinatuzuia kutokuwa tayari kuusikiliza ukweli na kujikinaisha kuwa tunatenda sawasawa. Ung’ang’anizi katika mali unatuondolea haiba ya kumvaa Kristo kama urithi wetu. Mtume Paulo katika somo la pili anatuambia kuwa katika Kristo “Mungu atavijumlisha vitu vyote, vitu vya mbinguni na vitu vya duniani.” Tunapoupindisha ukweli huu tunaingia katika kishawishi cha kuuchakachua utume tunapewa na kufanya mambo yetu. Tuupokee utume tunaopewa kwa kumweka Kristo kama chanzo na kielelezo chetu na pia ndiye kilele cha utume wetu, yaani kuufanya utume wetu unaoanzia katika Yeye na kuishia katika Yeye.

SALA: Ee Yesu utuepushe na tamaa ya mali katika utume wetu.

About mzigotv

Recommended for you