Mzigo-TV-728x90

Masomo ya misa

Masomo ya Misa Julai 30

By

on

Tumsifu Yesu Kristo. Karibu Katika Masomo ya Misa 30/07/2024

2024 JULAI 30: JUMANNE-JUMA LA 17 LA MWAKA

Mt. Petro Krisologi, Askofu na Mwalimu wa Kanisa
Rangi: Kijani

Zaburi: Juma 1

Somo 1. Yer 14:17-22

Macho yangu na yatiririke machozi, usiku na mchana; wala yasikome; kwa maana bikira, binti ya watu wangu, amevunjika mavunjiko makuu, kwa jeraha isiyoponyeka. Nikitoka kwenda shambani, tazama, wako huko waliouawa kwa upanga! Na nikiingia mjini, tazama, wamo humo wanaougua kwa sababu ya njaa! Maana nabii na kuhani, wote wawili, huenda huko na huko katika nchi, wala hawana maarifa. Je! Umemkataa Yuda kabisa? Roho yako imeichukia Sayuni? Mbona umetupiga, tusiwe na dawa ya kutuponya? Tulitazamia amani, lakini hayakuja mema yoyote; tulitazamia wakati wa kupona, na tazama, kufadhaika tu! Ee Bwana, tunakiri uovu wetu, na ubaya wa baba zetu; maana tumekutenda dhambi. Usituchukie, kwa ajili ya jina lako; usikifedheheshe kiti cha enzi cha utukufu wako; kumbuka, usilivunje agano ulilofanya nasi. Je! Katika vitu vya ubatili vya mataifa, kiko kitu kiwezacho kuleta mvua? Je! Mbingu zaweza kutoa manyunyu? Je! Si wewe, ee Bwana, Mungu wetu? Kwa sababu hiyo tutakungoja; kwa kuwa wewe umevifanya vitu hivi vyote.

Wimbo wa Katikati. Zab 79:8-9, 11, 13

1. Usikumbuke juu yetu maovu ya baba zetu,
Rehema zako zije kutulaki kama hima.
Kwa maana tumedhilika sana.

(K) Kwa ajili ya utukufu wa jina lako, utusaidie, ee Bwana

2.  Ee Mungu wa wokovu wetu utusaidie,
Kwa ajili ya utukufu wa jina lako.
Utuokoe, utughofirie dhambi zetu,
Kwa ajili ya jina lako. (K)

3. Kuungua kwake aliyefungwa na kuingia mbele zako,
Kwa kadiri ya uwezo wa mkono wako
Uwahifadhi wana wa mauti.
Na sisi tulio watu wako, na kondoo za malisho yako,
Tutashukuru milele;
Tutazisimulia sifa zako kizazi kwa kizazi. (K)

Injili. Mt 13:36-43

Yesu aliwaaga makutano, akaingia nyumbani; wanafunzi wake wakamwendea, wakasema, “Tufafanulie mfano wa magugu ya kondeni.”Akajibu, akasema,”Azipandaye zile mbegu njema ni Mwana wa Adamu; lile konde ni ulimwengu. Zile mbegu njema ni wana wa ufalme; na yale magugu ni wana wa yule mwovu; yule adui aliyeyapanda ni Ibilisi; mavuno ni mwisho wa dunia; na wale wavunao ni malaika. Basi, kama vile magugu yakusanywavyo na kuchomwa motoni; ndivyo itakavyokuwa katika mwisho wa dunia. Mwana wa Adamu atawatuma malaika zake, nao watakusanya kutoka katika ufalme wake machukizo yote, na hao watendao maasi, na kuwatupa katika tanuru ya moto; ndiko kutakuwako kilio na kusaga meno. Ndipo wenye haki watakapong’aa kama jua katika ufalme wa Baba yao. Mwenye masikio na asikie.”

TAFAKARI

TUKIKIRI DHAMBI TUNAKUWA IMARA: Mwanafalsafa Diogenes siku moja alitoka barabarani akibeba taa inayowaka. Mtu mmoja akamuuliza, unafanya nini? Diogenes akamjibu, natafuta mtu mwaminifu? Wakati mwingine tunaona mambo mengi ya kiulimwengu yakiendelea hata tunajiuliza wako watu wangapi waaminifu ulimwenguni humu? Uovu unamnyemelea kila mmoja wetu. Inafaa kuwa makini tukikesha katika muunganiko na Mungu ili kubakia waaminifu kwake. Tunapotambua tulikokosea tumgeukie Mungu anayetupokea kwa moyo wa huruma na mikono iliyo wazi. Tunapoukubali udhaifu wetu tunakuwa imara, “kwa maana ninapokuwa dhaifu ndipo ninakuwa na nguvu (2Kor 12: 10).” Tumepewa mfano wa watu wa Yuda wanaomkimbilia Mungu, “Ee Bwana, tunakiri uovu wetu, na ubaya wa baba zetu; maana tumekutenda dhambi. Usituchukie, kwa ajili ya jina lako; usikifedheheshe kiti cha enzi cha utukufu wako; kumbuka, usilivunje agano ulilofanya nasi.” Tujitahidi kuwa wenye haki kwa kutubu na kubakia waaminifu kwake.

Sala: Ee Bwana nipate kutambua vema uovu wangu na kuutubu.

About mzigotv

Recommended for you