Mzigo-TV-728x90

Masomo ya misa

Masomo ya Misa Julai 6

By

on

Tumsifu Yesu Kristo. Karibu Katika Masomo ya Misa 06/07/2024

2024 JULAI : ; JUMA  LA 13 LA MWAKA

Mt. Maria Goreti, Bikira na Shahidi
Rangi: Kijani

Zaburi:

Somo 1. Amo 9:11-15

Bwana asema hivi: siku hiyo nitaiinua tena maskani ya Daudi iliyoanguka, na kuziba mahali palipobomoka; nami nitayainua magofu yake, na kuyajenga kama siku za kale; wapate kuyamiliki mabaki ya Edomu, na mataifa yote yaitwayo kwa jina langu, asema Bwana, afanyaye hayo. Angalieni, siku zinakuja, asema Bwana, ambazo huyo alimaye atamfikilia avunaye, na yeye akanyagaye zabibu atamfikilia apandaye mbegu; nayo milima itadondoza divai tamu, na vilima vyote vitayeyuka. Nami nitawarejeza tena watu wangu Israeli waliohamishwa, nao wataijenga miji iliyoachwa maganjo, na kukaa ndani yake; nao watapanda mizabibu katika mashamba, na kunywa divai yake; nao watafanyiza Bustani, na kula matunda yake. Nami nitawapanda katika nchi yao, wala hawatang’olewa tena watoke katika nchi yao niliyowapa, asema Bwana, Mungu wako.

Wimbo wa Katikati. Zab 85: 9ab-14

1.  Nisikie atakavyosema Mungu Bwana,
Maana atawaambia watu wake amani.
Naam, na watauwa wake pia.
Bali wasiurudie upumbavu tena.

(K) Bwana anawaambia watu wake amani.

2.  Fadhili na kweli zimekutana,
Haki na amani zimebusiana.
Kweli imechipuka katika nchi,
Haki imechungulia kutoka mbinguni. (K)

3.   Naam, Bwana atatoa kilicho chema,
Na nchi yetu itatoa mazao yake.
Haki itakwenda mbele zake,
Nayo itazifanya hatua zake kuwa njia. (K)

Injili. Mt 9: 14-17

Wanafunzi wake Yohane walimwendea Yesu wakasema, Kwa nini sisi na Mafarisayo twafunga, bali wanafunzi wako hawafungi? Yesu akawaambia, Walioalikwa arusini wawezaje kuomboleza, muda bwana arusi akiwapo pamoja nao? Lakini siku zitakuja watakapoondolewa bwana arusi; ndipo watakapofunga. Hakuna mtu atiaye kiraka cha nguo mpya katika vazi kuukuu; maana kile kilichotiwa huondoa kipande cha lile vazi, na pale palipotatuka huzidi.  Wala watu hawatii divai mpya katika viriba vikuukuu; na kama wakitia, vile viriba hupasuka, divai ikamwagika, na viriba vikaharibika; bali hutia divai mpya katika viriba vipya, vikahifadhika vyote.

TAMBUA MABADILIKO NA KUYAPOKEA: Mwanadamu akikataa kupumua, hewa haimwadhibu wala kumfanyia chochote kile. Ila kwa namna hiyo tunajiadhibu au kujinyima hewa wenyewe. Mtu akiamua kupiga jiwe ngumi, jiwe haliiuadhibu mkono au ngumi ya huyo mtu bali tumejigonga na kujiumiza wenyewe. Kwa maelezo hayo tunapaswa kuelewa uhusiano walio nao Waisraeli na Mungu au uhusiano mdhambi anaoweza kuwa nao na Mungu. Mwanadamu anapaswa kuendelea kuwa tayari kubadilika kumwongokea Mungu. Wema wa Mungu unaendelea kubakia kama ulivyo, mwanadamu akiwa tayari kufanya mapenzi ya Mungu ni vema, ni kwa manufaa yake. Waisraeli walipokataa sheria ya Mungu, walijiadhibu wenyewe na sio Mungu aliyewaadhibu. Kuja kwa Kristo duniani kulianza kipindi kipya kwa Waisraeli, Masiha aliyeahidiwa amefika. Umuhimu wa kufunga kama ishara ya hamu, njaa na kungojea kuja kwake imepita. Sasa ni wakati wa kufurahi na kuushangilia ufalme wa Mungu ulioko kati ya watu. Hivyo ni wakati wa kumsikiliza Masiha kutambua yanayohitajika na kuyaishi.  

Sala: Ee Bwana utuwezeshe kutambua mabadiliko ya kweli na kuyapokea kwa furaha.

About mzigotv

Recommended for you