Mzigo-TV-728x90

Masomo ya misa

Masomo ya Misa Julai 7

By

on

Tumsifu Yesu Kristo. Karibu Katika Masomo ya Misa 07/07/2024

2024 JULAI 7: DOMINIKA YA 14 YA MWAKA
Rangi: Kijani
Zaburi:

Somo 1. Eze 2: 2-5

Bwana aliposema nami, roho ikaniingia, ikanisimamisha; nikamsikia yeye aliyesema nami. Akaniambia, Mwanadamu, nakutuma kwa wana wa Israeli, kwa mataifa wanaoasi, walioniasi mimi, wao na baba zao wamekosa juu yangu, naam, hata hivi leo. Na wana hao wana nyuso zisizo na haya, na mioyo yao ni migumu. Mimi nakutuma kwa hao; nawe utawaambia, Bwana Mungu asema hivi. Nao, kwamba watasikia, au kwamba hawataki kusikia, (maana ndio nyumba ya kuasi hao), hata hivyo watajua ya kuwa nabii amekuwako miongoni mwao. 

Wimbo wa Katikati. Zab 123

1. Nimekuinulia macho yangu,
Wewe uketiye mbinguni.
Kama vile macho ya watumishi
Kwa mkono wa Bwana zao.

(K) Macho yetu humwelekea Bwana, Mungu wetu. Hata atakapoturehemu.

2. Kama macho ya mjakazi
Kwa mkono wa bibi yake;
Hivyo macho yetu humwelekea Bwana, Mungu wetu.
Hata atakapoturehemu. (K)

3. Uturehemu, Ee Bwana, uturehemu sisi,
Kwa maana tumeshiba dharau.
Nafsi zetu zimeshiba mzaha wa wenye raha,
Na dharau ya wenye kiburi. (K)

Somo 2. 2 Kor 12: 7-10

Makusudi nisipate kujivuna kupita kiasi, kwa wingi wa mafunuo hayo nalipewa mwiba katika mwili; mjumbe wa Shetani ili anipige, nisije nikajivuna kupita kiasi. Kwa ajili ya kitu hicho nalimsihi Bwana mara tatu kwamba kinitoke. Naye akaniambia, Neema yangu yakutosha; maana uweza wangu hutimilika katika udhaifu. Basi nitajisifia udhaifu wangu kwa furaha nyingi, ili uweza wa Kristo ukae juu yangu. Kwa hiyo napendezwa na udhaifu, na ufidhuli, na misiba, na adha, na shida, kwa ajili ya Kristo. Maana niwapo dhaifu ndipo nilipo na nguvu. 

Injili. Mk 6: 1-6

Yesu alitoka, akafika mpaka nchi ya kwao, wanafunzi wake wakamfuata. Na ilipokuwa Sabato, alianza kufundisha katika sinagogi; wengi waliposikia wakashangaa, wakisema Huyu ameyapata wapi haya? na, Ni hekima gani hii aliyopewa huyu? na, Ni nini miujiza hii mikubwa inayotendeka kwa mikono yake? Huyu si yule seremala, mwana wa Mariamu, na ndugu yao Yakobo, na Yose, na Yuda, na Simoni? na maumbu yake hawapo hapa petu? Wakajikwaa kwake. Yesu akawaambia, Nabii hakosi heshima, isipokuwa katika nchi yake mwenyewe, na kwa jamaa zake, na nyumbani mwake. Wala hakuweza kufanya mwujiza wo wote huko; isipokuwa aliweka mikono yake juu ya wagonjwa wachache akawaponya. Akastaajabu kwa sababu ya kutokuamini kwao.

TAFAKARI

TUSIICHEZEE BAHATI YA MTENDE KUOTA JANGWANI
Upo msemo usemao: “usikihukumu kitabu kulingana na muonekano wake.” Maneno haya ya hekima yanatutaadharisha kuepa kufanya maamuzi kwa kufuata historia, mazoea au desturi fulani. Kwa hekima, mmoja anapaswa kufanya uchunguzi na ufuatiliaji wa kina kabla ya kutoa hukumu kuwa kitu fulani kinafaa au la! Au mtu fulani ni wa manufaa au la! Hapa tena tunakumbushwa msemo mwingine usemao: “uzuri wa mkakasi, kumbe ndani ni kipande cha mti”. Moja ya makosa ambayo wakati mwingi wanadamu hujutia ni kufanya maamuzi mbele. Wengi hushindwa kuipokea hali ya neema au baraka kutoka kwa wanaowaletea pengine kwa kuwajadili haiba yao, asili yao, uwezo wao kiuchumi au namna walivyowapokea katika jamii husika. Hapo ndipo utasikia maneno kama haya: “anatokea wapi huyu!” Yeye ni nani hadi atuambie hivyo” nk. Badala ya kuangalia ukweli na tija ya kile tuletewacho tunamjadili na kumhukumu mjumbe atuleteaye habari hiyo.
Masomo ya Dominika ya leo yanatutaadharisha kuepuka hukumu za namna hiyo na kujikuta tunaangukia katika kupoteza nafasi ya wokovu. Nafasi hii ni kama bahati ya mtende unaotaka kuota jangwani na jangwa hili ni nafsi yangu mimi na wewe ambao tumepoteza kabisa rutuba kiroho, tumemuasi Mwenyezi Mungu na tumeingia katika hali ya dhambi. Nabii Ezekieli anaifunua jamii hiyo katika somo la kwanza; jamii ambayo imekengeuka na kuingia katia uasi: “nakutuma kwa wana wa Israeli, kwa mataifa wanaoasi, walioniasi mimi.” Anatumwa kwenda kuitangaza habari njema ya wokovu bila kubabaishwa na chochote na kwamba hata wakikataa watakuja kutambua baadaye kuwa jambo hilo lilikuwa ni la manufaa kwao. Hapa tunauona uasi wa mwanadamu dhidi ya mwenyezi Mungu ulivyoshika mizizi tangu zamani.
Nabii Ezekieli anafanya utume wake wakati wa kipindi kigumu sana katika historia ya taifa la Israeli. Ni wakati ambapo waisraeli wamepelekwa utumwani (597K.K) kwa sababu ya uasi wao. Waisraeli walikuwa wamesahau baraka na fanaka walizopata wakati wa Mfalme Yosia kwa sababu waliishika vema torati. Wakaacha kuishika torati na kujikuta katika balaa hilo. Ezekieli anatumwa kuwafanyia unabii ili kuweza kutambua kosa lao kwani hata walipokuwa mateka bado walishindwa kuuona uasi wao. Uasi wa mwanadamu mara nyingi unamfanya asiwe tayari kusikiliza sauti ya wokovu inayomjia. Hii inaonesha wazi jinsi dhambi ilivyomuathiri mwanadamu hadi ndani kabisa kiasi cha kutokuwa tayari kufanya mabadiliko ya kiroho. Mwanadamu anapopotea dhambini anajifunga kabisa na kufurahia hali ya dhambi kana kwamba ndiyo namna njema ya kuishi.
Injili ya Dominika hii inaendelea kutuonesha hali hiyo. Watu wa Nazareti wanaletewa habari njema ya wokovu lakini wanashindwa kuipokea. Wanaanza kumchambua anayeleta Ujumbe badala ya kuupokea Ujumbe na kuufanyika kazi: “Huyu ameyapata wapi haya? Na Hekima gani hii aliyopewa huyu? Na, ni nini miujiza hii mikubwa inayotendeka kwa mikono yake?” Wananchi wenzake wa Nazareti wanaonesha wazi kutomtambua Kristo katika haiba yake; wanashindwa kuuona umasia wake na uwezo wa kimungu uliopo ndani mwake. Dharau, majivuno na kiburi cha kibinadamu kinafanya kucheza na bahati ya mtende kuota jangwani. “Ni mwana wa seremala”, moja ya kazi za kawaida kabisa na hivyo hatoki kwenye familia ya kutetemesha na hata hakusoma kupata Hekima kubwa hivyo ya kimungu; anapata wapi haya! Wanashindwa kuiona nafasi yake kama mwokozi wa wanadamu kutoka dhambini.
“Akastaajabu kwa sababu ya kutokuamini kwao.” Kristo anawashangaa jinsi wanavyotawaliwa na mawazo ya kibinadamu na kushindwa kutambua kuwa Mungu hutenda kupitia watu tunaoishi nao na tuliowazoea. Ni wazi kwamba wakati akikua hapo kijijini Nazareti walisikia habari fulani juu yake na namna mkono wa Mungu ulivyoonekana kutenda kazi pamoja naye tangu kuzaliwa kwake. Pili, Kristo alipofika hapo haikuwa kwao jambo geni kwa matendo mbalimbali aliyoyatenda mahali pengine. Sehemu nyingine ya Injili pacha inadhihirisha hilo. Kristo aliwaambia katika Injili ya Luka akisema: “hapana shaka mtaniambia mithali hii, Tabibu jiponye nafsi yako; mambo yote tuliyosikia kwamba yametendeka Kapernaumu, yatende na hapa katika nchi yako mwenyewe” (Lk 4:23). Hivyo walisikia juu ya ukuu wake na kwamba yeye ni nani lakini maamuzi mbele yaliwatawala: ameyapata wapi haya? Huyu si mtoto wa seremala na mama yake ndugu zake tunawajua. Hatuwezi kumsikiliza.
Mtume Paulo anatuonesha jinsi ambavyo Mungu anafikisha ujumbe wake hata kupitia vile ambavyo hatuvitegemei. Yeye binafsi alishangaa kwani pamoja na udhaifu aliokuwa nao katika kuongea bado Mungu alimchagua kuwafikishia wengine habari njema ya wokovu. Alimsihi Mungu amwondolee kilema hicho lakini alijibiwa “neema yangu inakutosha; maana uweza wangu hutimilika katika udhaifu” na hivyo akasema kwa furaha kwamba anajivunia udhaifu wake maana anapokuwa dhaifu ndipo anakuwa na nguvu. Ni sehemu ya maandiko matakatifu inayotufunulia jinsi Mungu anavyotenda kazi. Anapotupatia wito wa aina yoyote ni yeye anayetuwezesha kuukamilisha na hivyo tuutekeleze daima tukiwa tumeungana naye. Kwa upande mwingine ni dokezo kwetu kuwa tayari kuisikiliza suati yake kupitia watu mbalimbali bila kufanya hukumu kwani Mungu anamchagua anayemtaka ili kuitenda kazi yake ya wokovu.
Katika jamii tunayoishi tunategemea sana kuisikia sauti ya Mungu kutoka kwa watumishi wake. Lakini kwa bahati mbaya upepo wa dunia ya leo unatuondoa katika kuwasikiliza na hivyo mara nyingi tunabaki kuwajadili na pengine kujihalalishia uovu wetu. Tunajitetea katika dhamiri zetu kwa kisingizio cha anguko au makwazo uliyoyapata kutoka kwa mmoja wa watumishi wa Mungu. Leo hii tunaelekezwa kuelekeza mioyo yetu na akili zetu katika ujumbe unaotufikia bila kuangalia hali na haiba ya yeye anayetukifikishia kwani Mungu anachagua na kutufikishia ujumbe wake kupitia wenzetu tunaoishi nao. Ni yeye ambaye anatenda ndani mwao na kuwawezesha katika utume wao wa kinabii. Kwa nafasi nyingine tujipatie wajibu wa kuwaombea wenzetu wenye udhaifu ili kuongoka na kuimarika katika utakatifu.
Hivyo tuipokee sauti ya kinabii inayotujia kwa nafasi mbalimbali. Sauti hii ni sauti ya Mungu ambayo inanuia kuziamsha dhamiri zetu. Tuifanyie kazi sauti hiyo inayotaka kututoa katika uasi na kutupeleka katika uaminifu kwa Mungu. Tutambue kuwa sauti inayokujia kwa mmoja aliye karibu sana na wewe; sauti inayotoka kwa mwanafamilia, rafiki yako wa karibu au kwa yeye anayekufahamu kwa undani au mazingira yanayokuzunguka ni sauti yenye tija na inayonuia kukuelekeza vema kwa sababu yeye anayetoa sauti hiyo anakufahamu vema. Tusiichezee bahati ya mtende kuota jangwani! Kwani daima majuto ni mjukuu.

SALA: Ee Bwana utuepushe na kuhukumu watu kwa vyeo au nafasi zao kijamii.

About mzigotv

Recommended for you