Tumsifu Yesu Kristo. Karibu Katika Masomo ya Misa 08/07/2024
2024 JULAI 8: JUMATATU-JUMA LA 14 LA MWAKA
Wat.Hesperius na Zoa, Wafiadini
Rangi: Kijani
Zaburi:
Somo 1. Hos 2: 14-16, 19-20
Bwana asema hivi:”Angalia, mimi nitamshawishi, na kumleta nyikani, na kusema naye maneno ya kumtuliza moyo. Naye ataniitikia huko, kama siku zile za ujana wake, na kama siku ile alipopanda kutoka nchi ya Misri.Tena siku hiyo itakuwa, asema Bwana, utaniita ‘Ishi’, wala hutaniita tena ‘Baali.’Nami nitakuposa uwe wangu kwa milele; naam, nitakuposa kwa haki, na kwa hukumu, na kwa ufadhili, na kwa rehema. Nami nitakuposa kwa uaminifu; nawe utamjua Bwana. |
Wimbo wa Katikati. Zab 145:2-9
1. Ee Bwana wangu, Mfalme,nitakutukuza, (K) Nitalihimidi jina lako milele na milele. 2. Bwana ana fadhili,ni mwingi wa huruma, 3. Ee Bwana,kazi zako zote zitakushukuru, 4. Bwana ni mwenye haki katika njia zake zote, |
Injili. Mt 9:18-26
Yesu alipokuwa akiwaambia hayo, tazama, akaja jumbe mmoja, akamsujudia, akisema,”Binti yangu sasa hivi amekufa; lakini njoo, uweke mkono wako juu yake, naye ataishi.”Akaondoka Yesu, akamfuata, pamoja na wanafunzi wake. Na tazama, mwanamke aliyekuwa na ugonjwa wa kutoka damu muda wa miaka kumi na miwili, alikuja kwa nyuma, akaugusa upindo wa vazi lake. Kwa maana alisema moyoni mwake,”Nikigusa tu upindo wa vazi lake nitapona.” Yesu akageuka, akamwona, akamwambia,”Jipe moyo mkuu, binti yangu, imani yako imekuponya.”Yule mwanamke akapona tangu saa ile. Yesu alipofika nyumbani kwa yule jumbe, aliona wapiga filimbi, na makutano wakifanya maombolezo, akawaambia,”Ondokeni, kwa maana kijana hakufa, amelala tu.”Wakamcheka sana. Lakini makutano walipoondoshwa, aliingia, akamshika mkono; yule kijana akasimama. Zikaenea habari hizi katika nchi ile yote. |
TAFAKARI
IMANI INAPONYA: Jumbe anayewakilisha ombi lake kwa Kristo, amedhihirisha imani yake kwa kumwendea na kumwambia “Binti yangu sasa hivi amekufa; lakini njoo, uweke mkono wako juu yake, naye ataishi.” Mwanamke aliyekuwa mgonjwa kwa miaka kumi na mbili alijitafakari akatambua kwa imani kuwa akigusa vazi la Kristo atapona. Watu hawa wawili wanadhihirisha kuwa wana Imani kubwa. Mimi msomaji wa sasa je nadhihirisha Imani yangu kwa Kristo.Nadhiriki kulinganisha vazi la Kristo na Sakaramenti za Kanisa. Kama huyu mama kwenye Injili ya leo alivyoamua na kugusa vazi la Kristo kwa Imani nasi wakristo tunaweza kumfikia na kumgusa Kristo kwa Imani katika Sakaramenti tunazopokea. Tukifanya hivyo nguvu ya uponyaji kutoka kwenye Sakramenti za Kristo utatufikia kama ilivyomfikia huyu mama. Ulinganisho huu unaweza usiwe makini ila unatuwezesha kutambua zawadi ya neema inayopatikana kwa Sakramenti hizo, ukweli ni kuwa Kristo anapenda kumponya kila mmoja kama alivyomponya yule Mwanamke. Tuidhihirishe imani yetu. Sala: Ee Bwana utuwezeshe kutambua kuwa tunapata nguvu ya uponyaji wako katika Sakramenti. |