Mzigo-TV-728x90

Masomo ya misa

Masomo ya Misa Juni 10

By

on

Tumsifu Yesu Kristo. Karibu Katika Masomo ya Misa 10/06/2024

2024 JUNI 10 : JUMATATU-JUMA LA 10 LA MWAKA

Mt. Landri, Askofu
Rangi: Kijani
Zaburi: Juma 2

Somo 1. 1 Fal 17:1-6

Eliya Mtishbi, wa wageni wa Gileadi, akamwambia Ahabu, Kama Bwana, Mungu wa Israeli, aishivyo, ambaye ninasimama mbele zake, hakutakuwa na umande wala mvua miaka hii, ila kwa neno langu. Neno la Bwana likamjia, kusema, Ondoka hapa, geuka, uende upande wa mashariki, ujifiche karibu na kijito cha Kerithi kinachokabili Yordan. Itakuwa utakunywa maji ya kile kijito; nami nimewaamuru kunguru wakulishe huko. Basi akaenda akafanya kama alivyosema Bwana; kwa kuwa akaenda akakaa karibu na kijito cha Kerethi, kinachokabili Yordani. Kunguru wakamletea mkate na nyama asubuhi, na mkate na nyama jioni, akanywa maji ya kile kijito.

Wimbo wa Katikati. Zab 121:1-8

1. Nitayainua macho yangu niitazame milima;
Msaada wangu utatoka wapi?
Msaada wangu u katika Bwana,
Aliyezifanya mbingu na nchi.

(K) “Msaada wangu u katika Bwana,
aliyezifanya mbingu na nchi.”

2. Asiuache mguu wako usogezwe;
Asisinzie akulindaye;
Naam hatasinzia wala hatalala usingizi,
Yeye aliye mlinzi wa Israeli. (K)

3. Bwana ndiye mlinzi wako;
Bwana ni uvuli mkono wako wa kuume.
Jua halitakupiga mchana,
Wala mwezi wakati wa usiku. (K)

4. Bwana atakulinda na mabaya yote,
Atakulinda nafsi yako.
Bwana atakulinda utokapo na uingiapo,
Tangu sasa n ahata milele. (K)

Injili. Mt 5:1-12

Yesu alipowaona makutano, alipanda mlimani; na alipokwisha kuketi, wanafunzi wake walimjia; akafumbua kinywa chake, akawafundisha, akisema, Heri walio maskini wa roho; Maana ufalme wa mbinguni ni wao. Heri wenye huzuni; Maana hao watafarijika. Heri wenye upole; Maana hao watairithi nchi. Heri wenye njaa na kiu ya haki; Maana hao watashibishwa. Heri wenye rehema; Maana hao watapata rehema. Heri wenye moyo safi; Maana hao watamwona Mungu. Heri wapatanishi; Maana hao wataitwa wana wa Mungu. Heri wenye kuudhiwa kwa ajili ya haki; Maana ufalme wa mbinguni ni wao. Heri ninyi watakapowashutumu na kuwaudhi na kuwanenea kila neno baya kwa uongo, kwa ajili yangu. Furahini, na kushangilia, kwa kuwa thawabu yenu ni kubwa mbinguni; kwa maana ndivyo walivyowaudhi manabii waliokuwa kabla yenu.

DIRA YA KWENDA MBINGUNI: Mtu anaposafiri kuelekea mahali fulani anapaswa kujua mwelekeo anaopaswa kuufuata ili afike pale alipokusudia kufika. Bila kujua mwelekeo ni rahisi sana kupotea. Katika Injili ya leo Yesu anatupa dira ya kufuata ili tuweze kufika Mbinguni. Kwa upekee kabisa Yesu anatambua utajiri mkubwa uliopo katika umaskini wa roho yaani kujiona watupu ili kumruhusu Mungu aingie mioyoni mwetu. Katika heri tulizosikia Yesu anatupa mtazamo mpya katika maisha unaojumuisha watu wote bila ubaguzi pasipo kubagua maskini au tajiri. Hotuba ya Yesu inatualika kukuza fadhila za upole na unyenyekevu, huruma, usafi wa moyo na kuitunza amani. Kwa kukuza fadhila hizi tutaweza kutumia vizuri mali za ulimwengu huu kujipatia utakatifu. Tutaweza pia kutengeneza mahusiano mazuri baina yetu kwa upendo na umoja. Kwa kuitafuta amani tutajenga uhusiano mzuri kati yetu na wale tunaoishi nao na Mungu pia na hivyo kuwa kweli watoto wa Mungu.

SALA: Ee Mungu utujalie neema ya kuziishi Heri za Injili ili tuweze kukuona Wewe.

About mzigotv

Recommended for you