Muziki-TV-728x90

Masomo ya misa

Masomo ya Misa Juni 9

By

on

Tumsifu Yesu Kristo. Karibu Katika Masomo ya Misa 09/06/2024

2024 JUNI 9 : DOMINIKA YA 10 YA MWAKA

DOMINIKA YA 10 YA MWAKA
Rangi: kIJANI
Zaburi: Juma 2

Somo 1. Mwa 3: 9-15

Bwana Mungu alimwita Adamu, akamwambia, Uko wapi? Akasema, nalisikia sauti yako bustanini, naliogopa kwa kuwa mimi ni uchi; nikajificha. Akasema, Ni nani aliyekuambia ya kuwa u uchi? Je! Umekula wewe matunda ya mti niliyokuagiza usiyale? Adamu akasema, Huyo mwanamke uliyenipa awe pamoja nami ndiye aliyenipa matunda ya mti huo, nikala. Bwana Mungu akamwambia mwanamke, Nini Hili ulilofanya? Mwakamke akasema, Nyoka alinidanganya, nikala. Bwana Mungu akamwambia nyoka, Kwa sababu umeyafanya hayo, umelaaniwa wewe kuliko wanyama wote, na kuliko hayawani wote walioko mwituni; kwa tumbo utakwenda, na mavumbi utakula siku zote za maisha yako; nami nitaweka uadui kati yako na huyo mwanamke, na kati ya uzao wako na uzao wake; huo utakuponda kichwa, na wewe utamponda kisigino.

Wimbo wa Katikati. Zab 130: 1-8

1. Ee Bwana, toka vilindini nimekulilia,
Bwana, uisikie sauti yangu,
Masikio yako na yasikilize
Sauti ya dua zangu.

(K)Maana kwa Bwana kuna fadhili na kwake kuna ukombozi mwingi.

2. Bwana, kama wewe ungehesabu maovu,
Ee Bwana, nani angesimama?
Lakini kwako kuna msamaha,
Ili wewe uogopwe. (K)

3. Nimemngoja Bwana, roho yangu imengoja,
Na neno lako nimelitumainia.
Nafsi yangu inamngoja Bwana,
Kuliko walinzi waingojavyo asubuhi. (K)

4. Ee Israeli, umtarajie Bwana;
Maana kwa Bwana kuna fadhili,
Na kwako kuna ukombozi mwingi.
Yeye atamkomboa Israeli kwa maovu yake yote. (K)

Somo 2. 2 Kor 4: 13 – 5: 1

Kwa kuwa tuna roho ile ile ya imani; kama ilivyoandikwa, Naliamini, na kwa sababu hiyo nalinena, sisi nasi twaamini, na kwa sababu hiyo twanena; tukijua ya kwamba yeye aliyemfufua Bwana Yesu atatufufua sisi nasi pamoja na Yesu, na kutuhudhurisha pamoja nanyi. Kwa maana mambo yote ni kwa ajili yenu, ili neema hiyo ikiongezwa sana, kwa hao walio wengi, shukrani izidishwe, na Mungu atukuzwe. Kwa hiyo hatulegei; bali ijapokuwa utu wetu wan je unachakaa; lakini utu wetu wa ndani unafanywa upya siku kwa siku. Maana dhiki yetu nyepesi, iliyo ya muda wa kitambo tu, yatufanyia utukufu wa milele uzidio kuwa mwingi sana; tusiviangalie vinavyoonekana, bali visivyoonekana. Kwa maana vinavyoonekana ni vya muda tu; bali visivyoonekana ni vya milele. Kwa maana twajua ya kuwa nyumba ya maskani yetu iliyo ya dunia hii ikiharibiwa, tunalo jingo litokalo kwa Mungu, nyumba isiyofanywa kwa mikono, iliyo ya milele mbinguni.

Injili. Mk 3: 20-35

Mkutano walikusanyika tena, hata wao wenyewe wasiweze hata kula mkate. Jamaa zake walipopata habari wakatoka kwenda kumkamata; maana walisema, amerukwa na akili. Nao waandishi walioshuka kutoka Yerusalemu wakasema, Ana Beelzebuli, na kwa mkuu wa pepo huwatoa pepo. Akawaita, akawaambia kwa mifano, awezaje shetani kumtoa shetani? Na ufalme ukifitinika juu ya nafsi yake, ufalme huo hauwezi kusimama; na nyumba ikifitinika juu ya nafsi yake, nyumba hiyo haiwezi kusimama. Na kama shetani ameondoka juu ya nafsi yake, akafitinika, hawezi kusimama, bali huwa na kikomo. Hawezi mtu kuingia ndani ya nyumba ya mtu mwenye nguvu, na kuviteka vitu vyake, asipomfunga kwanza Yule mwenye nguvu, ndipo atakapoiteka nyumba yake. Amin, nawaambia, Dhambi zote watasamehewa wanadamu, na kufuru zao watakazokufuru zote; bali mtu atakayemkufuru Roho Mtakatifu hana msamaha hata milele; ila atakuwa ana dhambi ya milele; kwa vile walivyosema, Ana pepo mchafu. Wakaja mamaye na nduguze, wakasimama nje, wakatuma mtu kumwita. Na makutano walikuwa wameketi, wakimzunguka; wakamwambia, Tazama, mama yako na ndugu zako wako nje, wanakutafuta. Akawajibu, akisema, Mama yangu na ndugu zangu ni akina nani? Akawatazama wale walioketi wakimzunguka pande zote, akasema, Tazama, mama yangu na ndugu zangu! Kwa maana yeyote atakayeyafanya mapenzi ya Mungu, huyo ndiye ndugu yangu, na umbu langu, na mama yangu.

TAFAKARI.

“UTAKALO LIFANYIKE, DUNIANI KAMA MBINGUNI”
Uhusiano kati ya Mungu na mwanadamu ambao unajifunua katika suala zima la dini unamdai mwanadamu kuifuata na kuisikiliza sauti ya Mungu na si vinginevyo. Hii ni kwa sababu Mungu ndiye muumba wetu, Yeye ndiye chanzo cha maisha yetu na hivyo jinsi tulivyo na vyote tunavyomiliki ni kazi ya mikono yake. Bwana wetu Yesu Kristo alitufundisha sala iliyo bora kabisa, Sala ya Baba Yetu, na ndani mwake aliweka maneno ambayo yanatuelekeza katika kuyatafuta mapenzi ya Mungu: “Utakalo lifanyike duniani kama mbinguni”. Kifungu hiki katika sala hiyo kinatufunulia kwa namna fulani makusudi ya ukombozi wetu, unatufunulia habari njema aliyotumwa kuitangaza na ufalme wa Mungu. Hii ni kuwa na muunganiko na umoja kati ya Mungu muumba wetu na sisi viumbe vyake; yale anayonuia na kanuni alizotuwekea zibaki zinaheshimika huko juu mbinguni na hata hapa duniani.
Kadiri ya kanuni za kifizikia maji hufuata mkondo kuelekea kwenye mteremko na si vinginevyo. Hivi ndivyo inavyotegemewa kwa mwanadamu kuendana na mapenzi ya Mungu. Dhambi iliingia duniani pale mwanadamu alipojaribu kuubadili ukweli huu. Yeye ambaye ameumbwa kwa namna ya ajabu na cheo kikubwa kuliko viumbe wote alikengeuka na kupindisha maana ya uhuru wake na kujiamulia jinsi atakavyo na matokeo yake ni anguko kwa ubinadamu. Kiburi cha mwanadamu ambacho ni matunda ya kugeuza utii wake kutoka kwa Mungu na kumsikiliza shetani kilianza kuonesha athari zake mara moja. Mwanadamu alianza kujitenga na Mungu na pia mwanadamu mwenzake na uumbaji wote.
Somo la Kwanza limetuonesha namna mambo hayo yalivyotokea. Mwanadamu anaanza kumwogopa Mungu: “Nalisikia sauti yako bustanini, naliogopa kwa kuwa mimi ni uchi; nikajificha.” Ujasiri na kiburi chote cha kutaka kujilinganisha na Mungu unapotea. Mara moja anatambua nafasi yake kuwa si kitu mbele ya Mungu; bila Mungu anapungukiwa sana, anajiona yu mtupu. Anguko lake linaanza mara moja kwa sababu hakutaka kuyatimiza mapenzi ya Mungu. Utengano huo unaendelea hata baina ya wanadamu. Kila mmoja anajitengenezea uzio na kujitafutia ukamilifu: “Huyu mwanamke uliyenipa awe pamoja name ndiye aliyenipa matunda ya mti huo, nikala.” Si mimi niliyefikia hatua hiyo: kwanza ni wewe uliyeniletea balaa hilo kwa kuniwekea huyu mshawishi.
Furaha ya kumpata Eva aliyoonesha mwanzoni kabisa inapotea. Mwanadamu anatengana na mwanadamu mwenzake na pia mwanadamu anashindwa kukiri kosa lake. “Mwanamke akasema, Nyoka alinidanganya, nikala”. Mwanadamu anaendela kuliwa na uasi wake. Anajitenga na uumbaji, anaulaani uumbaji kuwa ndiyo sababu ya kuanguka kwake. Yote haya yanasababishwa na tendo moja la kutoyatii maagizo ya Mungu. Ingawa Maandiko Matakatifu hayaoneshi namna Eva alivyoagizwa kutokula matunda ya mti uliokatazwa lakini majadiliano yake na nyoka yalionesha dhahiri kuwa aliyapokea maagizo hayo na alifahamu madhara yake.
Kristo Mkombozi wetu alikuja kuturejeza katika njia sahihi. Katika Injili anaonesha kile ambacho kipo katika wokovu wa mwanadamu na kinaonesha mapinduzi makubwa katika jamii ya mwanadamu. “Kwa maana mtu yeyote atakayefanya mapenzi ya Mungu, huyo ndiye ndugu yangu, na umbu langu, na mama yangu.” Mapinduzi yake haya hayakupokeleka kirahisi na ndugu zake na jamii nzima. “Jamaa zake walipopata habari wakatoka kwenda kumkamata; maana walisema, Amerukwa na akili. Nao waandishi waloshuka kutoka Yerusalemu wakasema, Ana Beelzebuli, na, kwa mkuu wa pepo huwatoa pepo”. Linakuwa kwao neno gumu na wanashindwa kabisa kuuona mkono wa Mungu. Tujisumbue kidogo na kusoma sehemu iliyotangulia Injili ya leo ili kuelewa zaidi.
Ni siku ya sabato ambapo Yesu Kristo yupo katika Sinagogi na mbele yake anamwona mtu anayehitaji kuuonja upendo wa Mungu kwa uponyaji. Kitendo cha uponyaji siku ya sabato kinaleta nongwa na hivyo anatafutiwa ajali na kashfa inatengenezwa. Ndiyo tunaona kwa nini wanamsingizia kuwa anatumia nguvu ya Beelzebuli au nguvu za giza kutoa pepo. Ubinafsi wa kibinadamu unazuia upendo wa Mungu au mapenzi yake kwetu. Kwa kutambua umuhimu wa tendo hilo na kwa kufanya liendelee daima anachagua mitume kumi na wawili kwa kuendeleza kazi hiyo matokeo yake ni kuonekana kachanganyikiwa na kusingiziwa anatafuta ‘kiki’ kwa nguvu za giza. Kiburi cha mwanadamu kinajipenyeza ili kuzuia utendaji wa Mungu usifanyike kati ya watu. Wanaweka kauzibe ili kuendelea kufurahia na kuzipata faraja za ulimwengu huu ambazo ni za kupita na zenye kutuletea maangamizi.
Mtume Paulo anatupatia ujasiri: tusilegee katika imani na kutambua thamani iliyopo ndani mwetu. “Kwa hiyo hatulegei; bali ijapokuwa utu wetu wa nje unachakaa; lakini utu wetu wa ndani unafanywa upya siku kwa siku.” Katika ulimwengu kinzani wa leo huu ni Ujumbe wa kutia nguvu sana. Ni wazi mambo ya ulimwengu ambayo Paulo anatuambia ni ya muda wa kitambo tu; yale ambayo anatuambia pia tusiyaangalie na kuyakimbilia sababu yanaonekana, yanavutia, ni matamu na yanaonesha matumaini. Mambo haya mara nyingi hutuingiza katika utukufu wa muda na kuwa kinzani kuisikiliza sauti ya Mungu. Msuguano mkubwa katika ya dunia mamboleo na mafundisho na maelekezo ya Mama Kanisa ambayo hulenga katika kuustawisha utawala wa Mungu ni katika kusisitizia haya yanayoonekana na kushikika bila kuangalia yale yaliyofichika na yanayojikita katika ukweli.
Mara nyingi mwanadamu anauona utamu wa Mungu na maana ya uwepo wake katika mema tu. Hali ya mateso inapoanza kutuingia huishia katika uasi. Moyoni mwake huvutika sana na yale yanayotia moyo furaha na faraja. Kadhia na vurugu ya aina yoyote inapomuingia hufanya juhudi za kuiondoa kadhia hiyo. Ni sahihi kabisa kufanya juhudi hizi kwani vyote vinapaswa kufanywa katika hali ya ukamilifu na kutupatia furaha ya kweli. Mungu alipomaliza kazi ya uumbaji alivitazama vyote na kuona jinsi vilivyo vizuri na ukamilivu (rej. Mw 1:31). Changamoto ni jinsi ambavyo tunatafuta suluhisho la kadhia iliyopo mbele yetu. Mwanadamu analenga nini katika kutafuta suluhisho? Je, ni kuyatimiza mapenzi ya Mungu katika ukweli au tamaa zake tu?
Hiyo ndiyo changamoto inayowekwa mbele yetu katika Dominika hii. Hivyo tuombe neema ya Mungu kusudi kwanza tuitambue nafasi ya Mungu katika maisha yetu na hivyo kutafuta kuyatimiza mapenzi yake katika maisha yetu. Furaha ya kweli na ya kudumu inapatikana kwa kuunganika na Mungu katika ukweli. Tuepuke mambo ya nje nje na ya kupita; yale yanayotupatia ahadi ya faraja zisizodumu na hivyo tuikumbatie faraja itokayo kwa Mungu hata kama itapatikana kwa njia ngumu na isiyoshawishi na kutoa motisha. Tukumbuke daima kuwa “Barabara ndefu haikosi kona”, na tukivumilia hizo kona tutafika salama safari yetu.

SALA: Ee Mungu utuepushe na roho ya uasi.

About mzigotv

Recommended for you