Somo 1. 1 Fal 19: 19-21
Eliya aliondoka huko, akamkuta Elisha mwana wa Shafati, aliyekuwa akilima, mwenye jozi za ng’ombe kumi na mbili mbele yake, na yeye mwenyewe alikuwa pamoja na lile la kumi na mbili. Eliya akapita karibu naye, akatupa vazi lake juu yake. Naye akawaacha ng’ombe, akamfuata Eliya mbio, akasema, “Nipe ruhusa, nakuomba, nimbusu baba yangu na mama yangu, kisha mimi nitakufuata.” Akamwambia, “Enenda, urudi; ni nini niliyokutendea.” Akarudi akiacha kumfuata, akatwaa lile jozi la ng’ombe, akawachinja, akatokosa nyama zao kwa ile miti ya ng’ombe, akawapa watu, wakala, kisha akainuka, akamfuata Eliya, akamhudumia. |
Wimbo wa Katikati. Zab 16: 1b-2a, 5, 7-10
1. Mungu, unihifadhi mimi, (K) Bwana ndiye fungu la posho langu, na la kikombe changu. 2. Nitamuhimidi Bwana akiyenipa shauri, 3. Kwa hiyo moyo wangu unafurahi, |
Injili. Mt 5:33-37
Yesu aliwaambia wanafunzi wake: Mmesikia watu wa kale walivyoambiwa, Usizuru, ila mtimizie Bwana nyapo zako; lakini mimi nawaambia, Usiape kabisa; hata kwa mbingu, kwa maana ndicho kiti cha enzi cha Mungu; wala kwa nchi, kwa maana ndiyo pa kuwekea miguu yake; wala kwa Yerusalemu, kwa maana ndio mji wa Mfalme mkuu. Wala usiape kwa kichwa chako, maana huwezi kufanya unywele mmoja kuwa mweupe au mweusi. Bali maneno yenu yawe Ndiyo, ndiyo; Siyo; siyo; kwa kuwa yazidiyo hayo yatoka kwa yule mwovu. |
TAFAKARI
KUAMINIANA NI MUHIMU: Katika jamii za Agano la Kale hata mpaka kipindi cha Yesu, ili kuwaaminisha watu kuwa jambo linalosemwa ni la ukweli, lilisindikizwa na kiapo juu ya mtu mkubwa zaidi na ambaye angeweza kumwadhibu endapo baadaye angethibitika kuwa na uongo ndani yake. Mpaka sasa kwenye jamii na Kanisa kuna nyakati fulani zinadai kiapo na watu hufanya hivyo. Katika Injili ya leo Yesu anatufundisha umuhimu wa kusema ukweli bila ulazima wa kutumia kiapo. Anatuasa yale tunayosema yasukumwe na roho ya ukweli. Kama roho ya ukweli haipo ndani yetu hatutaona hata umuhimu wa kiapo. Badala ya kujikita kwenye viapo tujikite zaidi kwenye fadhila ya ukweli. Yesu mwenyewe ametuambia ukweli utatuweka huru. Hakuna atakayepata Neema kwa sababu ya kiapo bali Neema zitakuja kwa ukweli na haki. Kama hamna msukumo wa ndani wa kusema ukweli ni rahisi kabisa kuvunja viapo pia. SALA: Ee Yesu nijalie niweze kusimamia ukweli daima. |