SISI NI WASIA MBEGU NA MUNGU NDIYE MKUZAJI WA MBEGU Katika uhalisia wa ubinadamu wetu leo hii ipo kiu kubwa ya kutulizwa na uwepo wa Mungu na njaa ya kushibishwa na neno lake. Hii ni kwa sababu ulimwengu kinzani umetoa nafasi finyu kwa mwenyezi Mungu na kumtukuza zaidi mwanadamu. Tunashuhudia leo hii jinsi ambavyo mwanadamu anajitahidi kumtenganisha mwenyezi Mungu na maisha ya kawaida ya mwanadamu. Imani na tamaduni zetu zinatengwa kabisa kiasi kwamba hakuna muunganiko wa kile tunachokisikia katika nyumba za ibada na maisha halisia. Inakuwa sawa na livyosema mwandishi mmoja wa kiafrika kuwa: “Ewe mkristo mwafrika fukara unayevaa skapulari shingoni wakati umejifunga hirizi kiunoni.” Hali hii imemuingiza mwanadamu katika utumwa na mateso makubwa. Misiba na shuruba nyingi zinatokana na hali hiyo na hivyo kiu ya kuonja upendo wa Mungu inaongezeka siku hata siku. Katika hali hii sisi kama wanakanisa tunauona utume wetu wa kusia mbegu ya ufalme wa Mungu. Tunapaswa kuisia mbegu hiyo tukitambua kuwa inatoka kwa Mungu na Yeye mwenyewe ndiye atakayeikuza. Somo la kwanza linatupatia habari ya kuanza upya kwa taifa la Israeli baada ya utumwa wa Babeli. Nabii Ezekieli anatumia lugha ya picha inayoonesha kwa uwazi kabisa utendaji wa Mungu katika upya huo. Nabii Ezekieli anatoa utabiri wake wakati bado wakiwa utumwani Babeli, mahali ambapo waisraeli walipoteza hadhi kama taifa na hata kidini kukosa nafasi ya kuabudu sawasawa. Waisraeli waliingia katika hali hii baada ya kumuasi mwenyezi Mungu na kuacha kuzitii amri zake. Haya ni matokeo ya ukengeufu wao. Uaguzi huu unawainua tena; wale walionyenyekeshwa na kuwa wadogo kabisa watakuzwa upya. Huu ni uhakika kuwa kwa mwenyezi Mungu hakuna kilicho kidogo na kwa upande mwingine kwake hakuna kilichoharibika au kupotea kabisa kiasi cha kushindwa kurejeshewa hali yake. Ni uthibitisho wa upendo wa Mungu unaodumu milele. Mwanzo huu mpya unajionesha leo hii katika taswira ya Kanisa, chombo cha ukombozi wa mwandamu. Nabii Ezekieli analielezea Kanisa ambalo ni mwili wa Kristo kama ufalme ujao wa nyumba ya Daudi: “nami nitakitwaa kilele kirefu cha mwerezi … juu ya mlima wa mahali palipoinuka pa Israeli nitakipanda”. Kichipukizi hichi tangu kuanza kwake kilichipuka katika hali ya chini na duni kadiri ya macho ya kijamii. Jamii ya kiyahudi waliwaona kama watu wanaopotea na wasiodumu. Katika udogo na uduni huo Kanisa limeendelea kukua hadi leo. Hapa tunapaswa kuzama na kuona kilichodumu ni nini hasa; si uzuri wa majengo na ustadi wa taasisi zake bali ni neno la Mungu na imani thabiti. Hiki ndicho kinacholisimamisha Kanisa. Kazi ya Roho Mtakatifu ndani ya Kanisa inaendelea kufanya hai uwepo wa utajiri huu hadi leo. Ni ukumbusho sahihi kwetu sisi kwamba kazi ya uinjilishaji inahitaji kupandikiza mbegu ya neno la uzima; na bila kutikiswa na udogo au udhaifu wake tuwe na matumaini tele kwani Mungu mwenyewe ndiye atakayeikuza. Injili ya leo inaonesha mambo kadhaa. Injili inatupatia hakika ya ukuaji wa lile linalopandwa. Hata kama ukuaji wake haupo wazi lakini tutastaajabishwa na ukuaji wake. “Ufalme wa Mungu mfano wake ni kama mtu aliyemwaga mbegu juu ya nchi; akawa akilala na kuondoka, usiku na mchana, nayo mbegu ikamea na kukua, asivyojua yeye.” Kwa maneno mengine tunaalikwa kuwa na hali ya ustahimilivu, uaminifu, utulivu na matumaini. Mbegu imemea kwa sababu ni mbegu halisi iliyopandwa. Pia kwa hakika ni mbegu bora na imepandwa katika ukamilifu wake. Kazi ya uinjilishaji inatualika kwanza katika uaminifu wa kulifikisha neno la Mungu kama tulivyolipokea. Neno hili likipandwa hata kama halitaonekana au hata kama ni katika kundi dogo lina uhakika wa kumea. Pili tunaona kuwa namna mbegu inavyokuwa sisi hatufahamu lakini mwisho wa siku mbegu inakuwa. Huu ni uthibitisho wa utendaji wa Mungu katika kile chema ambacho kimeanzishwa kwa jina lake. Kwa maneno mengine tunaelekezwa katika ustahimilivu ambao hutupeleka katika ukomavu. Ni taadhari ya kuepuka hamu ya kuona mambo yanamea na kupendeza haraka haraka, hali ambayo utupeleka katika kukata tamaa kwani mara nyingi vitu vya namna hiyo huzimika ghafla kama moto nyikani. Ustahimilivu na hali ya matumaini hutoa nafasi ili mizizi ishike vizuri na baadaye kupata mmea ulio imara. Jambo lolote jema ambalo linaanza katika Mungu litawezeshwa na Mungu mwenyewe. Ufanisi wake haupimwi kwa vipimo vya kibinadamu kama kupata umaarufu na nguvu za kijamii bali ni katika kuufanya ukweli uenee na Ufalme wa Mungu kustawi. Ni changamoto kwa kizazi cha leo kinachovutika na mambo ya mlipuko na haraka haraka. Mambo mengi hayatoi fursa ya kutafakariwa vizuri, huanzishwa juu juu na mwisho wake hudumu kwa kitambo kidogo tu. Tukijiuliza sababu ya athari hii bado tunaliona suala la kumweka mwenyezi Mungu pembeni na kudhani kuwa sisi ndiyo asili na wawezeshaji wa yale tunayoyafanya. Hali hii hutushawishi kuingia katika mbinu ambazo mara zote hutoka kwa yule muovu, mbinu ambazo kwa hakika huvutia na kutia matumaini lakini kamwe hazilengi katika ukweli. Hizi ni zile mbinu ambazo hutafuta masuluhisho ya muda mfupi. Jamii yetu inapokumbana na changamoto nyingi ambazo kwa sehemu kubwa husababishwa na ukengeufu wa mwanadamu nafasi ya Mungu huwekwa kando katika kutafuta suluhisho lake. Njia za uovu hutumika kutafuta suluhisho la uovu. Ni vipi kipofu anaweza kumwongoza kipofu mwenzake? Tukirudi katika somo la kwanza tunaona jinsi ambavyo Waisraeli walianzishwa upya kwa mkono wa Mungu. Si wao waliojitoa utumwani bali ni Mungu mwenyewe ndiye anayewatoa na kuwafanya kustawi upya. Wema wote tulionao sisi wanadamu asili yake ni Mungu. Jambo jema tunalolianzisha linapaswa kuwa na Mungu kama asili yake. La muhimu kwetu ni uaminifu na uvumilivu ili likuwe na kumea na mwisho kutoa matunda. Ufalme wa Mungu “ni kama punje ya haradali … ingawa ni ndogo kuliko mbegu zote zilizo katika nchi, lakini ikiisha kupandwa hukua, ikawa kubwa kuliko miti yote ya mboga, ikafanya matawi makubwa.” Hatupaswi kuogopeshwa au kukatishwa tamaa na mwanzo wa jambo jema; pengine kwa udogo wake, udhaifu wake au upinzani unaolikabili. Mwisho wa siku kazi hii njema inayoanza na Mungu huzaa yaliyo mema. Mazao haya ni: “upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu, upole na kiasi” (Gal 5:22 – 23). Mtume Paulo anaunganisha ukuuji wa imani yetu na matendo mema tungalipo hapa duniani ili mwishoni kuungana na Mungu huko juu mbinguni. Mtume anaiona hali yetu kimwili hapa duniani ni kama kuwa mbali na Mungu lakini hali hii katika imani inapaswa kutufikisha baadaye kuungana na Mungu. Mtume anatuambia: “Ikiwa tupo hapa, au ikiwa hatupo hapa, twajitahidi kumpendeza yeye”, yaani Mwenyezi Mungu. Anatuasa kuyatumia maisha haya kama njia ya kuifanya mbegu iliyopandwa ndani mwetu ikue na kufikia ukamilifu. Wajibu wetu katika maisha ya kimaadili unapaswa kurandanishwa ni hicho kilichopandwa ndani mwetu na kutupatia tumaini la kukutana na Mungu. “Kwa maana imetupasa sisi sote kudhihirishwa mbele ya kiti cha hukumu cha Kristo, ili kila mtu apokee ijara ya mambo aliyoyatenda, kwamba ni mema au mabaya.”
SALA: Ee Mungu utujalie neema ya kustawisha mbegu ya Ufalme wako ndani yetu.
|