Somo 1. YbS 48:1-14
Nabii Eliya alisimama, kama moto, hata na neno lake likawaka kama tanuru. Yeye alileta njaa juu yao, na kwa juhudi yake akawapunguzia hesabu yao; kwa neno la Bwana akazifunga mbingu, na mara tatu kutoka huko akatelemsha moto. Jinsi ulivyotisha kwa miujiza yako! Aliye mfano wako ataona fahari. Aliyekufa ulimfufua katika mauti, kutoka kuzimu, kwa neno la Bwana. Ukawashusha wafalme mpaka shimoni, na watu wateule vitandani mwao. Ukapaka mafuta wafalme kwa kisasi, na nabii ili akufuate nyuma yako. Ulisikia makaripio huko Sinai, na hukumu za kisasi huko Horebu. Ukachukuliwa juu katika kisulisuli, katika gari la farasi wa moto. Ukaandikiwa kuwa utaleta makemeo, ili kutuliza hasira siku ile ya Bwana; kugeuza moyo wa baba umwelekee mwana na kuhusisha kabila za Israeli. Bila shaka wamebarikiwa wale waliokuona kwa macho, wakafa; lakini wewe umezidi kubarikiwa, kwa maana unaishi. Ndiye huyo Eliya aliyefunikwa kwa kisulisuli; hata na Elisha naye akajazwa roho yake; akazidisha ishara maradufu, na yale yaliyotoka kinywani mwake yalikuwa ya ajabu. Siku zake zote huyu pia hakushawishwa kwa kumwogopa mwenye kutawala, wala hakutiishwa na mtu yeyote. Hakukutokea neno lililokuwa gumu la kumshinda, hata na alipolala mautini mwili wake ulitoa unabii; kama alivyofanya miujiza katika maisha yake, kadhalika na katika mauti yake kazi zake zikawa za ajabu. |
Wimbo wa Katikati. Zab 97:1-7
1. Bwana ametamalaki, nchi na ishangilie, (K) Enyi wenye haki, mfurahieni Bwana. 2. Moto hutangulia mbele zake 3. Milima iliyeyuka kama nta mbele za Bwana, 4. Na waaibishwe wote waabuduo sanamu, |
Injili. Mt 6:7-15
Yesu aliwaambia wanafunzi wake: Mkiwa katika kusali, msipayuke-payuke, kama watu wa mataifa; maana wao hudhani ya kuwa watasikiwa kwa sababu ya maneno yao kuwa mengi. Basi msifanane na hao; maana Baba yenu anajua mnayohitaji kabla ninyi hamjamwomba. “Basi ninyi salini hivi; Baba yetu uliye mbinguni, jina lako litukuzwe, ufalme wako uje, mapenzi yako yatimizwe, hapa duniani kama huko mbinguni. Utupe leo riziki yetu. Utusamehe deni zetu, kama sisi nasi tuwasamehevyo wadeni wetu. Na usitutie majaribuni, lakini utuokoe na yule mwovu. Kwa maana mkiwasamehe watu makosa yao, na Baba yenu wa mbinguni atawasamehe ninyi. Bali msipowasamehe watu makosa yao, wala Baba yenu hatawasamehe ninyi makosa yenu. |
TAFAKARI
MSAMAHA NI MUHIMU KWA MAISHA YA MKRISTO: Injili ya leo inatufundisha kuwa ili sala yetu ipokelewe na Mungu, haitegemewi kurudia maneno mengi na kwa kupayuka ila inategemea wema huruma na upendo wa Mungu kwetu. Mungu anapenda mafanikio yetu na anafahamu mahitaji yetu hata kabla hatujamwomba. Sala ya Baba yetu aliyotufundisha inatuingiza katika uhusiano wa ndani na Mungu ndiyo maana tunamwita Mungu Baba. Kwa sala hii Mungu anajibu kilio cha wote wamwombao mahitaji yao mbalimbali. Kwa sala hii tunamwomba Mungu ili mahisiano yetu naye na wenzetu yawe mazuri kwani mara kadhaa tunakoseana na kuharibu mahusiano kati yetu na Mungu na kati yetu na ndugu zetu. Njia pekee ya kurudisha mahusiano hayo ni msamaha. Tupokee mwaliko wa kusameheana sisi kwa sisi tunapokoseana. Kwa kusali sala hii, tunampa Mungu kipimo cha kutumia katika kutoa msamaha kwetu, hivyo tumwombe Mungu tuweze kusamehe bila mipaka ili nasi tuweze kupokea msamaha huo mbele yake.
|
SALA: Ee Mungu utujalie moyo wa msamaha.