Mzigo-TV-728x90

Masomo ya misa

Masomo ya Misa Juni 21

By

on

Tumsifu Yesu Kristo. Karibu Katika Masomo ya Misa 21/06/2024

2024 JUNI 21 : IJUMAA-JUMA LA 11 LA MWAKA

Aloisi Gonzaga, Mtawa
Rangi: Kijani
Zaburi: Juma 

Somo 1. 2 Fal 11:1-4, 9-18, 20

Athalia, mama yake Ahazia, alipoona ya kuwa mwanawe amekufa, akainuka, akawaharibu wazao wote wa kifalme. Ila Yeosheba, binti wa mfalme Yehoramu, umbu lake Ahazia, akamtwaa Yoashi mwana wa Ahazia, akamwiba miongoni mwa hao wana wa mfalme waliouawa, yeye na mlezi wake, na kuwatia katika chumba cha kulala; wakamficha usoni pa Athalia, basi kwa hiyo hakuuawa. Alikuwako pamoja naye, amefichwa nyumbani mwa Bwana, miaka sita. Naye Athalia akaitawala nchi. Hata mwaka wa saba Yehoyada akatuma, na kuwaleta wakuu wa mamia, wa Wakari, na wa walinzi, akawaleta kwake ndani ya nyumba ya Bwana; akapatana nao, akawaapisha nyumbani mwa Bwana, akawaonyesha huyo mwana wa mfalme. Nao wakuu wa mamia wakafanya sawasawa na yote aliyowaamuru Yehoyada kuhani; wakawatwaa kila mtu watu wake, hao watakaoingia sabato, nao watakaotoka sabato, wakaja kwa Yehoyada kuhani. Naye yule kuhani akawapa wakuu wa mamia mikuki na ngao zilizokuwa za mfalme Daudi, zilizokuwamo nyumbani mwa Bwana. Walinzi wakasimama, kila mtu na silaha zake mkononi, kutoka pembe ya kuume ya nyumba mpaka pembe ya kushoto ya nyumba, kando ya madhabahu na nyumba, wakimzunguka mfalme pande zote. Ndipo akamleta nje mwana wa mfalme, akamvika taji, na kumpa ushuhuda; wakamfanya mfalme, wakamtia mafuta; wakapiga makofi, wakasema, Mfalme na aishi.  Na Athalia alipoisikia sauti ya walinzi na ya watu, aliingia kwa watu nyumbani kwa Bwana; akatazama, na tazama, mfalme amesimama karibu na nguzo kama ilivyokuwa desturi, nao wakuu na wapiga baragumu karibu na mfalme; na watu wote wa nchi wakafurahi, wakapiga baragumu. Ndipo Athalia akararua mavazi yake, akalia, Fitina! Fitina! Naye Yehoyada kuhani akawaamuru wakuu wa mamia, majemadari wa jeshi, akawaambia, mtoeni kati ya safu; naye ye yote amfuataye mwueni kwa upanga. Kwani kuhani akasema, Asiuawe nyumbani mwa Bwana. Basi wakampisha njia; akaenda kwa njia ya kuingia kwa farasi nyumbani mwa mfalme; akauawa huko. Kisha, Yehoyada akafanya mapatano kati ya Bwana na mfalme na watu, ili wawe watu wa Bwana; tena kati ya mfalme na watu. Watu wote wa nchi wakaiendea nyumba ya Baali, wakaiangusha; madhabahu zake na sanamu zake wakazivunja-vunja kabisa, na Matani kuhani wa Baali wakamwua mbele ya madhabahu. Na Yehoyada kuhani akaweka maakida juu ya nyumba ya Bwana. Basi watu wote wa nchi wakafurahi, na mji ukatulia. Naye Athalia wakamwua kwa upanga karibu na nyumba ya mfalme. 

Wimbo wa Katikati. Zab 132: 11-14, 17-18

1. Bwana amemwapia Daudi neno la kweli,
Hatarudi nyuma akalihalifu,
Baadhi ya wazao wa mwili wako
Nitawaweka katika kiti chako cha enzi.

(K) “Bwana ameichagua sayuni,
ameitamani akae ndani yake. “

2. Wanao wakiyashika maagano yangu,
Na shuhuda nitakazowafundisha;
Watoto wao nao wataketi
Katika kiti chako cha enzi milele. (K)

3. Kwa kuwa Bwana ameichagua Sayuni,
Ameitamani akae ndani yake.
Hapo ndipo mahali pangu pa raha milele,
Hapo nitakaa kwa maana nimepatamani. (K)

4. Hapo nitamchipushia Daudi pembe,
Na taa nimemtengenezea masihi wangu.
Adui zako nitawavika aibu,
Bali juu yake taji yake itasitawi. (K)

Injili. Mt 6:19-23

Yesu aliwaambia wanafunzi wake: Msijiwekee hazina duniani, nondo na kutu viharibupo na wevi huvunja na kuiba; bali jiwekeeni hazina mbinguni, kusikoharibika kitu kwa nondo wala kutu, wala wevi hawavunji wala hawaibi; kwa kuwa hazina yako ilipo, ndipo utakapokuwapo na moyo wako. Taa ya mwili ni jicho; basi jicho lako likiwa safi, mwili wako wote utakuwa na nuru.  Lakini jicho lako likiwa bovu, mwili wako wote utakuwa na giza.  Basi ile nuru iliyomo ndani yako ikiwa giza; si giza hilo!

TAFAKARI

TUWEKEZE SASA KWA MAISHA YAJAYO: Katika maisha yetu ya kawaida tunashauriwa kipato chetu tunachokipata tukigawe katika sehemu tatu, yaani kwa ajili matumizi ya kila siku, kwa ajili ya maendeleo na kwa ajili ya akiba. Yesu leo anatukumbusha kutumia muda wa sasa kwa ajili ya kuandaa hazina au akiba ya maisha yajayo. Anatutahadharisha kuwa tusijilimbikizie mali na kuwa tusiwe vipofu katika kuitazama dunia. Anatufundisha kuwa yote tutendayo sasa yajengwe katika msingi wa Mungu. Tukijenga katika msingi wa kibinadamu tutapata hasara kubwa bali tukijenga katika msingi wa Kimungu tutapata faida sasa na baadaye. Hivyo tumpe Mungu nafasi ya kwanza ayatawale maisha yetu. Kazi zetu, biashara zetu, ratiba zetu, familia zetu visichukue nafasi ya Mungu bali Mungu apewe nafasi ya kwanza na mengine yatafuata baadaye. Kwa kufanya hivi hazina yetu itakuwa salama muda wote. Ili haya yaweze kutendeka ni lazima kuwa na jicho linaloweza kuona kwa mtazamo wa kimungu.

Sala: Ee Mungu nijalie nikupe nafasi ya kwanza katika Maisha yangu.

About mzigotv

Recommended for you